Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi milioni 10.5 walipatiwa huduma ya afya mwaka 2018.

Wakimbizi wakiwa katika kituo cha afya kilichoko katika kambi yao ya Nakivale nchini Uganda
IRIN/Samuel Okiror
Wakimbizi wakiwa katika kituo cha afya kilichoko katika kambi yao ya Nakivale nchini Uganda

Wakimbizi milioni 10.5 walipatiwa huduma ya afya mwaka 2018.

Wahamiaji na Wakimbizi

Licha ya viwango vya juu vya ukimbizi na hamahama duniani, bado takribani wakimbizi milioni 10.5 walipatiwa huduma ya afya kupitia miradi ya afya kwa umma na mipango ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti yenye takwimu za mwaka za tathmini  ya afya ya umma duniani zilizotolewa hii leo na UNHCR ikiangazia hali ya afya, lishe, maji, huduma za kujisafi na usafi kwa wakimbizi, wasaka hifadhi na jamii zinazowahifadhi katika  mataifa 51.

Kamishna Msaidizi wa  UNHCR anayehusika na operesheni, George Okoth-Obbo amesema wakati asilimia 84 ya wakimbizi wote wanahifadhiwa katika nchi zinazoendelea, ambako huduma za  msingi tayari zimezidiwa uwezo, mifumo ya afya ya kitaifa inahitaji usaidizi ili kuhakikisha wakimbizi na wenyeji wao wanapata huduma muhimu za kuokoa maisha yao.

Wakimbizi wa Nigeria ambao walikimbia machafuko katika maeneo yao, wakiwa wamepanga mstari kwa ajili ya maji katika kambi ya Minawao kaskazini mashariki mwa Cameroon (Februari 2019)
UN Photo/Eskinder Debebe)
Wakimbizi wa Nigeria ambao walikimbia machafuko katika maeneo yao, wakiwa wamepanga mstari kwa ajili ya maji katika kambi ya Minawao kaskazini mashariki mwa Cameroon (Februari 2019)

Mafanikio  yaliyopatikana

Ripoti imetaja mafanikio  yaliyopatikana kutokana na huduma hizo  kuwa ni pamoja na kupungua kwa viwango vya vifo vya watoto wakimbizi wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Kiwango hicho kimepungua licha ya ongezeko la wimbi la wakimbizi kutoka Myanmar, Sudan Kusin na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Halikadhalika, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya wakimbizi kujumuishwa kwenye mifumo ya matibabu ya kitaifa huku nchi nyingine zikichukua hatua kujumuisha wakimbizi kwenye mifumo ya bima ya afya na hifadhi ya  jamii.

Katika mataifa 37 yanayohifadhi wakimbizi, kundi hilo linaweza kupata tiba dhidi ya Kifua Kikuu, Virusi Vya Ukimwi na Malaria kama ilivyo kwa wenyeji.

UNHCR inasema pia juhudi ziliendelea mwaka jana kusongesha na kuwezesha huduma za kina za afya ya uzazi ikiwemo zile za mama na mtoto pamoja na uzazi wa mpango.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo,  katika asilimia 80 ya mataifa yaliyofanyiwa utafiti, UNHCR inasaidia huduma za afya ambapo asilimia 90 ya wajawazito wakimbizi walijifungua watoto wao kwenye vituo vya afya vyenye wakunga walio na stadi, hali ambayo ni msingi wa kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Je kuna changamoto zozote kusaidia afya ya wakimbizi?

Hata hivyo ripoti inasema bado kuna maeneo yenye pengo kama vile kudhibiti magonjwa ya milipuko miongoni mwa wakimbizi ikitaja milipuko kama vile ugonjwa wa dondakoo na surua Bangladesh na kipindupindu nchini Uganda.

Kwa mantiki hiyo, shirika hilo linasema kwa kuzingatia mwenendo wa ukimbizi unavyozidi kushamiri duniani, UNHCR inahitaji msaada zaidi kwa huduma zake za afya.

Hadi katikati ya mwaka huu wa 2019, UNHCR imepokea asilimia 30 tu ya bajeti ya dola bilioni 8.6 ya kusaidia huduma za kuokoa maisha kwa wakimbizi walioko kwenye mataifa 131.