Acheni kushambulia watoto- UNICEF

Watoto, wakati wote, wanahitaji amani na ulinzi, hiyo ni kauli iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto la UNICEF, Henrietta H. Fore.
Amesema kuanzia Jamhuri ya Afrika ya Kati hadi Sudan Kusini, Syria hadi Afghanistan mashambulizi dhidi ya watoto kwenye maeneo ya vita yamekuwa yakiendelea bila kusita katika miezi minne ya kwanza ya mwaka huu.
Bi. Fore ametolea mfano Yemen ambako watoto zaidi ya 220 waliuawa na wengine 330 walijeruhiwa kutokana na mgogoro huo.
Nako Sudan Kusini, takriban watoto milioni 2.6 wamelazimishwa kuhama makazi yao, huku watoto zaidi ya milioni 1 wanakabiliwa na utapiamlo.
Ameongeza kuwa makundi yanayohasimiana, bila kujali kuwajibishwa, yameendelea kupuuza sheria za kulinda raia ikiwemo watoto kwenye maeneo ya vita.
Kama hiyo haitoshi, shule na hospitali zinalengwa huku vizuizi vikiwekwa kuzuia ufikishaji wa misaada ya kibinadamu.
Mkuu huyo wa UNICEF amesema watoto wanahitaji amani na ulinzi wakati wowote na ametaka kukomeshwa mara moja kwa tabia ya kuwashambulia watoto.