Sheria mpya Italia yatumbukiza nyongo operesheni za uokozi Mediteranea

6 Agosti 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limeelezea wasiwasi wake mkubwa hii leo kufuatia uamuzi wa bunge la Italia wa kubadili kuwa sheria amri ya usalama inayoweka adhabu kali kwa boti na watu wanaofanya msako na operesheni kwenye bahari ya Mediteranea.

UNHCR inasema kwa mabadiliko hayo, tozo la faini kwa boti binafsi ambazo zinafanya operesheni za uokozi au ambazo hazitaheshimu zuio la kuingia kwenye maji yaliyo chini ya mamlaka ya Italia, imeongezeka hadi Yuro milioni 1 pamoja na chombo husika kukamatwa.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi, Charlie Yaxley amewaeleza waandishi wa habari kuwa “bado UNHCR ina wasiwasi kuwa kwa kuweka tozo la faini au adhabu kwa boti hizo kunaweza kuzuia operesheni za uokozi zinazofanywa na vyombo binafsi vya majini wakati huu ambapo serikali za  Ulaya zimejitoa kwa kiasi kikubwa katika operesheni za uokozi kwenye maeneo ya kati ya bahari ya Mediteranea.”

Bwana Yaxley amesema azma na ubinadamu ambavyo vinachochea operesheni za uokozi havipaswi kuharamishwa au kunyanyapaliwa.

Halikadhalika UNHCR inasema mashirika ya kiraia hayapaswi kulazimishwa kuhamishia wahamiaji waliookolewa kwenda kwa walinzi wa pwani ya Libya au kuelekezwa kuwapeleka Libya.

“Hali mbaya na tete ya usalama, na mapigano yanayoendelea pamoja na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na watu kushikiliwa kiholela ni ushahidi dhahiri kuwa watu hawapaswi kupelekwa Libya,” amesema Bwana Yaxley.

UNHCR imetoa wito kwa serikali kuzingatia majadiliano ya hivi karibuni mjini Paris, Ufaransa ambamo kwayo yalianzisha mpango wa muda na unaotabirika kwa watu wanaoshushwa kutoka katika meli za uokozi, mpango ambao pia unatambua wajibu wa pamoja baina ya nchi wa kukidhi mahitaji yao.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud