Ulaji wa nyama za binadamu na ubakaji ulishamiri Kasai, DRC Ripoti

3 Julai 2018

 

Magenge ya wahalifu kubaka wanawake kwa makundi, ulaji wa nyama za binadamu pamoja na ukatajiwa viungo vya siri vya binadamu  na kuvivaa kama vidani vya mapambo, ni miongoni mwa visa vya uhalifu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu  uliofanywa huko  nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.

Visa hivyo vimetajwa katika ripoti ya uchunguzi uliofanywa na jopo la kimataifa la wataalamu lililotumwa na Umoja wa Mataifa kuchunguza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye maeneo ya Kasai.

Ripoti hiyo iliyosheheni mahojiano kutoka kwa waathirika, asasi za kiraia na  wataalam wa haki za binadamu imebaini kuwa pande zote katika mgogoro nchini humo yakiwemo magenge ya wahalifu, vikundi viliyojihami pamoja  na vikosi vya usalama walihusika na  ukiukwaji wa haki za binadamu kwa maelfu ya watoto, wanawake na watu wasiojiweza katika jamii mbambali nchini humo.

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein akizungumzia ripoti hiyo amesema ukiukwaji wa haki za binadamu nchini DRC umeongezeka kutoka  visa 2332 mwaka jana hadi  visa 2858 mwaka huu.

UNHCR/John Wessels
Familia nzima ikikimbia ghasia huko Kamonia, jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

 

Zeid ametiwa hofu zaidi na ghasia kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kwenye eneo hilo la Kasai ambapo vikundi vilivyojihami vya Nyatura na Mayi-Mayi vinaendeleza ghasia.

Na huko kaskazini mashariki migogoro kati ya Hema na Lendu ambako uchomwaji wa vijiji na mauaji vimesababisha ukimbizi wa mamioni ya raia katika   nchi jirani ya Uganda.

Bwana Zeid amegusia pia sera mpya inayojadiliwa na serikali ya DRC inayolenga kuweka vikwazo zaidi kwa wanaharakati wa haki za bindamu nchini humo akisema sera hizo zinakiuka haki ya kukusanyika na uhuru wa kujieleza kwa wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Bacre Waly Ndiaye ambaye aliongoza jopo la wataalamu wa kimataifa amesema hali ya haki za binadamu inatisha ambapo baadhi ya vitendo hivyo vinawezakuwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. “ zaidi ya wanaume na watoto  186 kutoka kijiji kimoja waliuawa kwa kutenganishwa viwiliwili vyao na Kamuina Nsapu ambaye ni mkuu wa genge la wahalifu. 

Na wengi wao ni wale wanaopelekwa kwenye mapigano na wanamgambo waliojihami wenyewe wakiwa na fimbo, huku wanawake wakibakwa, mamia ya maelfu ya watu wakilazimika kukimbia makwao,” amesema Bwana Ndiaye.

Wataalam wameongeza kuwa miili ya waathirika  huzikwa katika makaburi ya pamoja, huko viungo vyao vikianikwa kama mapambo kwa wahalifu kwa lengo la kutishia jamii mbalimbali ya vijijini.

Kupitia azimio la haki za binadamu nambari 35/33, ofisi ya haki za binadamu ilisimamia uchunguzi  uliofanya na vikosi vya usalama vya Congo pamoja na kundi la wataalam wachunguzi wa uhalifu wa kimataifa, na mashahidi mbalimbali.

Kwa upande wake  Abdoul Azizi Thioye ambaye ni kaimu mkuu wa ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini DRC amesema ijapokuwa  kuna changamoto za  ukiukwaji wa haki za bindamu,  bado kuna hatua iliyopigwa katika uimarishaji wa usalama kupitia makubaliano ya desemba mwaka 2016 kati ya serikali na upinzani kuhusu uimarishaji wa usalama katika kuelekea katika uchaguzi.

Wakimbizi kutoka kijiji cha Kasaï jimbo la Kasai wakisubiri mgao wa chakula.(Picha:Joseph Mankamba/OCHA-DRC)
Wakimbizi kutoka kijiji cha Kasaï jimbo la Kasai wakisubiri mgao wa chakula.(Picha:Joseph Mankamba/OCHA-DRC)

Katika mjadala huo, serikali ya DRC iliwakilishwa na Maria Ange Mushobekwa ambaye ni waziri wa haki za binadamu DRC ambaye amesema wanatambua kuwa baadhi ya wawakilishi wa kiserikali na kimataifa wanapaza sauti zisizo na ukweli wowote kuhusu haki ya za binadamu nchini humo.

Hata hivyo amesema tayari serikali inachunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu huko Kasai.

Washiriki wa mjadala huo wametoa mapendekezo kadhaa ikiwemo wito  kwa serikali ya DRC  kutoa ushirikiano na ofisi  ya haki za binadamu katika kuwafikisha wahusika wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu mbele ya vyombo vya dola ili sheria ichukuwe mkondo wake.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter