Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misri mwachieni huru binti wa Al-Qaradawi na mumewe

Kikao cha Baraza la haki za binadamu. (Picha:OHCHR/Facebook)

Misri mwachieni huru binti wa Al-Qaradawi na mumewe

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa wito kwa serikali ya Misri imwachie mara moja Ola Al- Qaradawi na mumewe Hosam Khalaf ambao wameswekwa korokoroni kiholela tangu wakamatwe tarehe 30 mwezi juni mwaka jana.

Bi Qaradawi ambaye ni binti wa mwanaharakati Sheikh Yusuf Al-Qaradawi, raia wa Misri anayetuhumiwa kuwa na uhusiano na chama chaMuslim Brotherhood cha nchini Misri, anashikiliwa kwenye gereza lenye mazingira mabaya zaidi huko Misri huku akinyimwa fursa ya kutembelewa na ndugu zake.

Msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu Liz Throsell amesema jopo la wataalam wa haki za binadamu wamekuwa  wakipigania kuachiwa huru kwa Bi. Al-Qaradawi na mume wake, huku likisisitiza kuwa kukamatwa kwao kulikuwa kinyume cha sheria.

Wamesema kuendelea kuongezwa mara kwa mara kwa amri ya kuwekwa korokoroni kwa siku 45 kumesababisha kukiukwa kwa haki zao sambamba na mchakato wa haki wa kesi.

Jopo hilo limesema linatambua kuwa tayari Bi. Al-Qaradawi ameanza mgomo wa kula chakula na wanaamini kuwa anashikiliwa kutokana na uhusiano na baba yake mzazi.

Wamesema wanaelewa kuwa afya yake inazidi kudorora na hivyo wamesihi mamlaka zihakikishe kuwa haki yake ya kupata huduma ya afya, inazingatiwa sambamba na huduma za kimwili na kisaikolojia.

Na kwa mantiki hiyo wamesihi serikali ya Misri imwachie huru Bi Al-Qaradawi na mumewe bila masharti yoyote.