Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutenga familia kwa misingi ya uhamiaji kunadhuru ukuaji wa watoto

Mama na mwanae kwenye mpaka wa Rio Grande kati ya Mexico na McAllen, katika jimbo la Texas.
Picha UNICEF/Adriana Zehbrauskas
Mama na mwanae kwenye mpaka wa Rio Grande kati ya Mexico na McAllen, katika jimbo la Texas.

Kutenga familia kwa misingi ya uhamiaji kunadhuru ukuaji wa watoto

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia  watoto, UNICEF pamoja na jopo la watalaam wa haki za binadamu   wamesema agizo jipya la Rais wa Marekani la tarehe 20 mwezi huu la kuzuia kutenga watoto na wazazi wao, haujafafanua  kwa kina  hatma ya maelfu ya watoto walioko vizuizini kwa madai ya kuingia nchini humo  kinyume cha sheria.

Wakizungumza na wandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, hii leo kuhusu uamuzi huo wa kusitisha  sera ya kutovumilia uhamiaji kinyume cha sheria kwa  wanaosaka hifadhi ambao wanakuja na  watoto wao, wadau hao wamesema hatua hiyo, haijaeleza  kwa kina utatuzi wa suala hilo ikiwemo hatma wa watoto hao pamoja na familia zao.

Christophe Boulierac ambaye ni msemaji wa UNICEF amesema  kwamba, sisi tunapinga uamuzi wa kutenga wazazi na watoto kwa misingi ya sheria ya uhamiaji”.

Kwa pamoja wametoa wito kwa  serikali ya Marekani kuwaachia huru watoto hao kutoka vifungoni na kuwaunganisha pamoja na familia zao kwa maslahi ya mtoto, na haki za watoto kwa mujibu wa sheria ya haki za binadamu .

Wamesema mgawanyiko huo  kati ya watoto na wazazi wao  umefanyika bila ya taarifa au maandalizi.

Wazazi na watoto hawajaweza kuzungumza na hadi sasa  wazazi  hawajapata taarifa kuhusu mahali walipo watoto wao, kitu ambacho ni kiyume na sheria ya Umoja wa Mataifa ya kuhusu uhuru na umoja wa familia,” wameongeza.

Jumatatu iliyopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alisema kikanuni wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuchukuliwa kama binadamu kwa kupewa  heshima, kwa mujibu wa sheria ya kimataifa iliyopo.

Naye kamishna mkuu   wa haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein katika ufunguzi wa kikao cha 38 cha Baraza la haki za binadamu  huko Geneva Jumatatu ya wiki hii,  alisema suala la kuwatenga watoto na wazazi  kwa misingi  ya hali ya uhamiaji ni unyanyasaji wa watoto unaoweza kusababisha madhara makubwa katika ukuaji wa watoto .