Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iran sitisha hukumu ya kifo dhidi ya Panahi

Nchi zinatakiwa kuachana na adhabu ya kifo kwani OHCHR inasema ni kinyume na haki za binadamu. (Picha:http://bit.ly/2y6kIrf)

Iran sitisha hukumu ya kifo dhidi ya Panahi

Haki za binadamu

Wataalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamerejelea wito wao kwa Iran ifute hukumu ya kifo dhidi ya Ramin Hossein Panahi, ambaye hukumu amepangiwa kunyongwa baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Bw. Panani ambaye ni raia wa Iran mwenye asili ya kikurdi, alipangwa kunyongwa mwezi mei, lakini  adhabu yake iliahirishwa.

Yafahamika kuwa ombi la kupitia upya hukumu yake lilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Iran mwishoni mwa mwezi Mei, na hukumu dhidi yake ilipelekwa kwenye ofisi inayohusika na unyongaji.

Kupitia taarifa yao iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi, wataalamu hao akiwemo Anges Callamard wamesema ijapokuwa wanshukuru kuahirishwa kwa hukumu hiyo mwezi uliopita, bado kuna dalili kuwa mahakama Iran ina nia ya kutekeleza  hukumu ya kunyongwa kwa Bw. Panahi huku ikipuuza wito wa kukomesha hukumu ya kifo, na kuhakikishiwa kuwa anapewa haki katika hukumu yake.

Wataalamu hao wamesema kuna kasoro nyingi za kisheria kuhusiana na kesi hiyo, ikiwa ni pamoja na ripoti ya kuteswa kwa  Bw. Panahi ,kunyimwa haki yake ya msingi ya kupewa mwanasheria na ukosefu wa matibabu.

Wataalam pia walisisitiza wasiwasi wao kwamba mashtaka dhidi ya Bw. Panahi hayakuzingatia viwango vya kimataifa, ambavyo vinasema kwamba adhabu ya kifo lazima   iendane kwa kesi za mauaji ya makusudi.

Bw. Panahi alikamatwa mwezi Juni mwaka jana kwa tuhuma ya kuwa  mwanachama wa kikundi Kikurdi la Komala.

Alipatikana na hatia kwa kosa la kupambana na vikosi vya  serikali, na kuhukumiwa kifo na Mahakama ya Kimapinduzi nchini Iran mwezi Januari mwaka huu.