ECA inaamini usafiri bora wa treni ndio muafaka kwa Afrika

18 Juni 2018

Tume ya kiuchumi kwa ajili ya Afrika, ECA leo imesema inaamini kwamba usafiri wa treni indio utakuwa dawa mujarabu ya kukabiliana na adhya ya usafiri barani Afrika.

Kwa mujibu wa tume hiyo gharama na uchumi wa nchi nyingi za Afrika kuyumba yumba kumefanya kuhitajika kwa muundo mpya wa uwekezaji utakaojumuisha sekta za umma na binafsi, na kuwa na eneo huru la biashara Afrika lililozinduliwa mapema mwaka huu kutaongeza mahitaji ya usafiri kama wa treni.

Akifafanua kuhusu hilo katibu mtendaji wa ECA Vera Songwe amesema anaamini kwamba usafiri wa treni utakuwa muafaka kwa bara la Afrika kwani mfumo wa usafiri wa sasa hautoshelezi na Afrika inahitaji mfumo mkubwa zaidi na unaokidhi mahitaji.

Amesema kwa sasa Afrika ina reli ya kilometa 1 kwa kila eneo la kilometa 400, na kuna mifumo aina tatu tofauti hali ambayo inaweka mazingira yasiyowiana na kuongeza gharama katika bara hilo.

Hata hivyo ECA imesema azma hiyo itakuwa na gharama kubwa  kwa mfano kufufua reli baina ya Ethiopia na Djibout kunagharimu zaidi ya dola bilioni 4, reli mpya baina ya Nairobi na Mombasa nchini Kenya imeongeza deni la nje la nchi hiyo kwa asilimia 17, huku kubadili mfumo wa reli ya Afrika Kusini kuwa wa kisasa zaidi kunahitaji dola bilioni 110.

Kwa sababu ya gharama hizi na hali ngumu ya uchumi wa mataifa mengi ya Afrika, Katibu mtendaji wa ECA anaamini kwamba mfumo bunifu wa biashara na uwekezaji katika mitaji unahitajika.

Songwe ameeleza kwamba ubia baina ya sekta za umma na binafsi utatoa fursa kwa sekta binafsi ya uwekezaji salama na wa muda mrefu, na kwa sekta za umma amesema zitafaidika kwa usimamizi, ubunifu, kiufundi na uwezo wa kifedha wa sekta binafsi.

Katika mkutano uliofanyika wiki iliyopita mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini , Songwe alizungumzia makubaliano ya mfumo wa reli ya Luxembourg na kueleza kwamba  makubaliano hayo yataanza kutekelezwa rasmi 2019 na ili kuwezesha uwekezaji wa miundombinu ya aina hiyo nchi zinatakiwa kuridhia muafaka huo.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo “ni muhimu kwa mfumo wa reli barani Afrika na chachu ya mustakhbali wa uchumi wa bara hilo”

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter