Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya haki za binadamu duniani si shwari- Zeid

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’aad al-Hussein. UN/Jean-Marc Ferré

Hali ya haki za binadamu duniani si shwari- Zeid

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amehutubia kikao cha 38 cha Baraza la haki za binadamu huko Geneva, Uswisi na kusema kuwa hali ya haki hizo duniani kote sasa si shwar. 

Ikiwa ni hotuba yake ya mwisho mbele ya Baraza hilo kabla ya kung’atuka kwenye wadhifa huo baadaye mwaka huu, Bwana Zeid amegusia hali ya haki za binadamu katika mataifa mbalimbali.

Ameonyesha wasiwasi wake mkubwa kuhusu mashambulio dhidi ya bandari ya Hudaydah nchini Yemen, mashambulizi yanayoongozwa na Saudi Arabia na Falme za kiarabu.

(sauti ya zeid ra’ad al hussein)

 “Yanaweza kusababisha majeruhi mengi kwa raia wa kawaida na kuwa na athari kubwa kwa misaada ya kibinadamu inayopitia bandari hiyo kwa ajili ya kusaidia mamilioni kadhaa ya watu.”

Kuhusu Syria kamishna Zeid amesema kuwa ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu umeshudiwa nchini humo akisema mhusika mkuu ni serikali na washirika wake, huku akinyooshea kidole makundi yenye misimamo mikali.

Ameangazia pia Afrika akiitaja Burundi, akisema kuwa licha ya serikali ya nchi hiyo mwaka jana kukubali kushirikiana na kundi la watalaam  waliopewa idhini na baraza hilo la haki za binadamu , bado kundi hilo lilifukuzwa na hadi sasa halijafanikiwa kurejea.

 (sauti ya zeid ra’ad al hussein)

  “Kwa muda huohuo  hali ya haki za kibinadamu inazidi kuzorota  nchini kote ambako makundi ya kiraia hayapewi nafasi kutoa kauli zao. Na uamuzi wa kubadilisha katiba ya nchi kupitia kura ya maoni  mwezi jana umezusha wasiwasi wa masuala ya haki za kibinadamu kama vile madai ya kukamatwa kiholela kwa watu 44 kunaweza kuzidisha hali kuwa mbaya zaidi. Natoa wito kwa serikali kurejesha mfumo wa mazungumzo  na makundi yote ya kibinadamu ya kimataifa.”

Zeid pia amegusia suala la uzalendo akisema uzalendo kamili unahusika na kujenga jamii ambazo zinavumiliana na kuishi pamoja kwa amani.