ICC yamfutia Bemba makosa ya uhalifu wa kivita na dhidi ya binadamu

8 Juni 2018

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague Uholanzi  imemfutia makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, Makamu wa zamani wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Jean- Piere Bemba.

Uamuzi huo unafuatia rufani iliyowasilishwa na Bemba baada ya kuhukumiwa dhidi ya makosa hayo na mengine mwaka 2016.

Jaji aliyeongoza kesi hyo Christine Van den Wyngaert amesema  baada ya kusikiliza pande zote majaji watatu kati ya watano waliafiki kutupilia mbali makosa hayo mawili wakisema kuwa vipengele vingi havikuzingatiwa wakati hukumu ilipotolewa.

Hata hivyo Jaji Wyngaert  amesema mtuhumiwa  atasalia kifungoni kutokana namakosa mengine aliyopatikana na hatia ambayo ni kuingilia utawala akisubiri uamuziwa suala hilo utakaotolewa ndani ya siku chache na majaji Sanji Mnasenono na Piotr Hofmanski wanaosimamia kesi hiyo.

Uamuzi huo utawezesha kufahamu iwapo Bemba atatakiwa kuachiwa huru au kuendelea kusalia kifungoni kwa makosa hayo ya kuingilia utawala wa sheria na kuzuia haki.

Mnamo machi 21 mwaka 2016 Bw. Bemba alikutwa na hatia kama kamanda wa jeshi ya kutekeleza makosa mawili ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, ambayo ni mauaji na ubakaji, makosa matatu ya uhalifu wa vita ukijumuisha mauaji, ubakaji na uporaji.

Makosa hayo yalitekelezwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR mwezi Oktoba mwaka 2002 na Machi 2003.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud