Wataalam wa UN wakaribisha uamuzi wa mahakama Guatemala

22 Oktoba 2018

Uamuzi wa mahakama nchini Guatemala kuwa watu wa jamii ya asili ya Lxul Mayans niwaathirika wa mauaji ya kimbari pamoja na mauaji dhidi ya binadamu, ni tukio la kihistoria  ambalo linatoa mfano bora wa juhudi za kusaka haki siyo tu nchini humo pekee bali pia kikanda na kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Geneva Uswisi na  watalaam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Watalaam hao wamesema kuwa , “uamuzi wa mahakama unahakikisha  kuwa  mateso na fedheha waliyopitia watu hao wa kabila la lxil chini ya mikono ya wanajeshi wa Guatemala inakuwa sawa na makosa ya mauaji ya kimbari na pia uhalifu dhidi ya ubinadamu.”

 Wameongeza kuwa wanafurahia ushindi na hatua iliyopigwa  katika kutafuta ukweli, na pia vita dhidi ya kutowajibishwa na vilevile  kufufua yaliyojiri  nchini Guatemala katika kipindi cha  kati ya mwaka 1969 hadi 1996 ambapo watu wanaokadiriwa 200,000 walipoteza maisha yao.

Uamuzi wa mahakama katika kesi kuhusu vifo vya watu 1,771, wengi wao wakiwa ni kabila la lxil yaliyotokea kati ya  1982 hadi 1983, umethibitisha kuwa  jeshi la Guatemalalilitumia nguvu kupindukia dhidi ya raia wa ikiwemo kuua, kutesa, ukatili wa kingono na pia kuwalazimisha watu hao kuhama makwao.

 Watalaam wanasema kuwa hatua hii ya mahakama ni kuthibitisha kile kilichokuwa kimeamuliwa  Mei 10 mwaka 2013 ambapo mahakama ya mwanzo ilimkuta na hatia  kiongozi wa wakati huo, Jose Efrain Rios Montt kwa makosa hayo hayo ilhali ilimuondolea mashtaka  aliyekuwa mkuu wa kikosi cha ujasusi Jose  Mauricio Rodriguez Sanchez.

 Uamuzi huo  wa mwanzo,ulibatilishwa baadaye na mahakama ya katiba kwa kudai kuwepo  kile ilichoita ni dosari. Kesi ilirejelewa tena  mwaka wa 2017, lakini ikadumazwa na kifo cha Rios Montth mnamo  April 2018.

Hata hivyo kesi dhidi ya mkuu wa zamani wa ujasusi iliendelea  na kukamilika baada ya kumuondolea mashtaka katika hukumu iliyosomwa Oktoba 18.

Watalaam wamesema kuwa kilichobaki ni serikali kuweza kuwatambua na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika na visa hivyo kama hatua moja ya kufariji familia  na waathirika kuona kama  wanapata haki.

 Pia wamesifu ujasiri na uvumilivu vilivyodhihirishwa na  wale waliotaka kuona haki ikitendekana  kwa kipindi cha miongo mitatu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud