Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Niko Somalia kuunga mkono mchakato wa amani: DiCarlo

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisiasa akiwa ziarani nchini Somalia alipokutana na Rais wa shirikisho la Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed Farmaajo
Picha ya UM/Omar Abdisalan
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisiasa akiwa ziarani nchini Somalia alipokutana na Rais wa shirikisho la Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed Farmaajo

Niko Somalia kuunga mkono mchakato wa amani: DiCarlo

Amani na Usalama

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisiasa, yuko ziarani nchini Somalia ambako amekutana na uongozi wa serikali na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNSOM.

Rosemary DiCarlo, anayezuru kwa mara ya kwanza nchini Somalia kama mkuu wa idara ya masuala ya siasa ya Umoja wa Mataifa DPA na msaidizi wa Katibu Mkuu, leo amekuwa na mikutano na Rais wa shirikisho la Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed Farmaajo katika mji mkuu Mogadishu, ili kusisitiza nia ya Umoja wa Mataifa ya kuwasaidia watu wa Somalia na serikali yao, lakini pia kujadili masuala ambayo ni kipaumbela kwa pande zote mbili.

Katika ziara hiyo Bi DiCarlo ameambatana na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu nchini Somalia na mkuu wa UNSOM Michael Keating.

Akizungumza baada ya mkutano na Rais Farmaajo, Bi DiCarlo amesema lengo kuu la ziara yake ya kwanza mashinani ni kuunga mkono mchakato wa kisiasa na amani unaoendelea pamoja na kutafiti ni vipi Umoja wa Mataifa unaweza kuisaidia vizuri Somalia kukabiliana na changamoto lukuki kuanzia masuala ya kibinadamu, usalama hadi ajenda ya kisiasa.

Amepongeza kazi inayofanywa na kamati ya shirikisho ya katiba nchini humo na kongamano la kitaifa la katiba lililofanyika hivi karibuni ambalo limesisitiza ujumuishwaji, ushirikiano na muafaka na kutaka kukamilishwa kwa mchakato wa kutathimini katiba ndani ya mwaka mmoja.

Ameongeza kuwa Somalia iko katika wakati muhimu sana hivi sasa na kutathimini katiba kunaweza kuwa chachu kubwa ya mabadiliko. Amesisitiza kwamba mshikamano kwa Wasomali ni muhimu katika kupiga hatua za amani, kupunguza machafuko, kukomesha itikadi kali, kushughulikia changamoto za kibinadamu na kuwanusuru Wasomali.

Kisha Bi Dicarlo akakutana na naibu mwakilishi maalumu wa mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika, Simon Mulongo, na kupongeza kazi inayofanywa vikosi vya muungano wa Afrika nchini humo AMISOM, hasa kwa ari na kujitolea kwao kuhakikisha nchi hiyo inapata amani ya kudumu.