Somalia yasonga mbele, licha ya changamoto za kisiasa, kiuchumi na kiusalama- Haysom

3 Januari 2019

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Haysom, leo amehutubia Baraza la Usalama la Umoja huo jijini New York, Marekani akitoa tathmini ya hali ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi.

Mathalani amesema tayari nchi hiyo imeweka misingi ya kusonga mbele kwenye nyanja hizo kwa mwaka 2019 kwa kuwa tayari mipango ipo dhahiri akitolea mfano usimamizi wa uchaguzi wa kikanda mwaka huu wa 2019 sambamba na mchakato wa kisiasa hususan mapitio ya katiba akisema mambo hayo yatabaini iwapo Somalia itasonga mbele au la.

Akifafanua mchakato wa kisiasa, Bwana Haysom ametaja rasimu ya sheria ya uchaguzi akisema tayari imewasilishwa Baraza la Mawaziri ikiwa na marekebisho kutoka mashirika ya kiraia, vyama vya kisiasa na jamii ya kimataifa.

“Kuchelewa kuwasilisha bungeni rasimu hiyo ya sheria ya uchaguzi itakuwa ni kupoteza fursa muhimu kwa mujibu wa ahadi ya serikali na ratiab ya mchakato wa uchaguzi,” amesema Bwana Haysom, akipongeza hata hivyo tume ya huru ya taifa ya uchaguzi, NIEC kwa kuendelea na maandalizi ya uandikishaji wa wapiga kura, kuajiri watendaji wapya, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi na kupanga maeneo ya upigaji kura. Amesema hadi sasa vyama 35 vimeshasajiliwa.

Usalama bado Al Shabaab ni tishio; kiuchumi serikali imejizatiti kukusanya mapato

Bwana Haysom ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya Umoja wa mataifa ya usaidizi wa Somalia, UNSOM amegusia pia suala la usalama akisema kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab, kimesalia kuwa chanzo kikubwa cha ukosefu wa usalama kwenye taifa hilo la pembe la Afrika licha ya harakati za kukidhoofisha.

Hata hivyo amepongeza jeshi la Somalia na vikosi vya Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM kwa kuweza kuvunja uwezo wa kikundi hicho kufanya mashambuliz makubwa zaidi ya kutumia vilipuzi vya kutengeneza.

Kuhusu  uchumi, amepongeza hatua ya serikali ya shirikisho ya kuongeza uwezo wake wa kukusanya mapato akisema  mwezi Septemba mwaka jana, mapato ya ndani yalikuwa na ziada ya dola milioni 8, ikimaanisha kuwa asilimia 56 ya bajeti ya serikali kuu ya dola milioni 340 kwa mwaka 2019 itatokana na mapato ya ndani.

Tunashukuru usaidizi lakini uhuru wetu uheshimiwe- Balozi Osman

Katika mkutano huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Somalia kwenye Umoja wa Mataifa balozi Abukar Dahir Osman ametumia hotuba  yake kuelezea hatua walizochukua ikiwemo kudhibiti rushwa pamoja na kuimarisha uwezo wa vikosi vya usalama.

Hata hivyo amekumbusha wajumbe wa Baraza kuwa Somalia ni nchi huru na inataka uhuru huo uheshimiwe na mambo yake ya ndani yasiingiliwe.

Naye Mwakilishi Maalum wa Muungano wa Afrika nchini Somalia na mkuu wa AMISOM Balozi Francisco Madeira amesema licha ya  changamoto zilizopo nchini humo bado serikali imeweza kupiga hatua katika masuala ya siasa jumuishi, haki na usalama pamoja na kujikwamua kiuchumi.

Amesihi Umoja wa Mataifa na wadau wengine waendelee kupatia Somalia ushirikiano ili hatimaye iweze kufikia ndoto yake ya kuwa taifa lenye amani, utulivu na maendeleo.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter