Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Somalia kwa mabadiliko ya kiusalama:UNSOM

Maisha nchini Somalia kwa muda mrefu yamekuwa magumu kutokana na vita isiyokoma.
OCHA/Cecilia Attefors
Maisha nchini Somalia kwa muda mrefu yamekuwa magumu kutokana na vita isiyokoma.

Heko Somalia kwa mabadiliko ya kiusalama:UNSOM

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika, Muungano wa Ulaya, serikali ya Uingereza na serikali ya Marekani wamekatribisha hatua iliyochukuliwa na waziri mkuu wa Somalia Hassan Ali Khaire kuwaeleza wadau hao wa kimataifa kuhusu mabaddiliko katika sekta ya usalama nchini humo na miapango inachukuliwa na serikali kuendelea kuimarisha hali ya usalama Somalia.

Taarifa iliyotolewa na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM inasema jumuiya ya kimataifa imetiwa moyo na ari ya serikali ya shirikisho ya Somalia ya kutekeleza mabadiliko ya lazima ya kiusalama, kiuchumi na kisiasa na imehimiza msaada wake kwa ajili ya mabadiliko hayo.

UNSOM imesema jumuiya ya kimataifa inatarajia majadiliano zaidi wakati mikutano ya msimu wa chipukizi ya Benki ya Dunia na shirika la fedha duniani IMF, itakayofanyika mwezi April.

Pia wadau hao wamesema wanatarajia maamuzi muhimu kwa minajili ya msaada kwa mpango wa muungano wa Afrika nchini Somalia , AMISOM hasa ikijiandaa kukabidhi jukumu la ulinzi kwa wizara ya ulinzi ya Somalia.

Jumuiya hiyo ya kimataifa imesema ina imani ya utekelezaji kikamilifu wa mabadiliko hayo nchini Somalia ambayo yatachangia kuleta utulivu na ustawi kwa watu wa Somalia na ukanda mzima.

Wamewachagiza wadau wote kusaidia na kuunga mkono juhudi za pamoja ili kuisaidia serikali ya Somalia kufikia azima ya mabadiliko hayo kupitia mchakato jumuishi wa majadiliano.