Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwekeze katika elimu na ajira ili tuokoe vijana dhidi ya itikadi kali :Lajčák

Miroslav Lajčák rais wa mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akihutubia mdahalo wa vijana
Picha ua UN /Manuel Elias
Miroslav Lajčák rais wa mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akihutubia mdahalo wa vijana

Tuwekeze katika elimu na ajira ili tuokoe vijana dhidi ya itikadi kali :Lajčák

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika mdahalo wa vijana ulioandaliwa na rais wa mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuwahamasisha vijana katika masuala ya elimu, ajira na pia mazungumzo kuhusu athari za kutumbukia kwenye itikadi kali

Katika ufunguzi wa mdahalo huo Rais wa Baraza hilo Miroslav Lajčák alianza kwa kuonyesha umuhimu wa ushirikishwaji na pia ujumuishwaji wa vijana wa kila rika katika masuala ya maendeleo endelevu ili kuweza kuwaandaa kushiriki vyema katika mustakabali wa maisha yao.

Rais huyo wa Baraza Kuu la UN amegusia mambo muhimu matatu , ikiwa ni pamoja na elimu ambapo amesema vijana wanatakiwa kuandaliwa mazingira mazuri ya elimu ili waweze kukabiliana na changamoto za baadae katika uchumi wa dunia.

Na katika suala la pili ambalo ni ajira Bw. Lajčák amegusia changamoto wanazokabiliana nazo vijana wengi katika soko la ajira , ambalo kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kazi duniani ILO, asilimia kubwa ya vijana duniani hususani katika nchi zenye uchumi wa chini, tatizo la ajira ni kuzungumkuti hivyo maandalizi ni muhimu ili kuwapata fursa ya ajira bora.

Jambo la tatu ni suala la athari za vijana kutumbukia katika ilikadi za kigaidi, akisema kutokana na kwamba idadi kubwa ya vijana duniani wana umri wa chini ya miaka 25 na wengi wao wanakosa fursa ya elimu na ajira, ni rahisi kurubuniwa na watu wenye itikadi kali ili waweze kijiunga na makundi ya kigaidi.

Bwana Lajčák amesema suala la vijana kujiunga na makundi ya kigaidi ni suala mtambuka na linatakiwa kuzungumzwa kwa kuwashirikisha vijana katika midahalo kama wa leo ili kuweza kubadilishana mawazo na kujua nini kifanyike ili kuepukana na vitendo hivyo katika jamii.

 

Jayathma Wickramanayake mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya vijana akihutubia mdahalo wa vijana
Picha ya UN /Manuel Elias
Jayathma Wickramanayake mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya vijana akihutubia mdahalo wa vijana

Mdahalo huo uliwajumuisha vijana wengine mashuhuri kama Jayathma Wickramanayake ambaye ni Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya vijana ambaye pia amepongeza juhudi za vijana kama Mohamed Sidibe, kutoka Sierra Leone ambaye baada ya kukosa elimu akiwa mtoto na kulazimishwa kujiunga na vikundi vya wanamgambo kama askari mtoto akiwa mdogo, alifanikiwa kurudi shule na sasa ni mwanaharakati wa Umoja wa Mataifa katika kuwahimiza vijana kuendelea na elimu .

Bwana Lajčák amekumbusha vijana kuwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha maazimio yenye malengo ya kuwahimiza na kuwashirikisha vijana katika

malengo ya maendeleo endelevu ikiwa ni pamoja na kuepukana na masuala ya ugaidi, amani na maendeleo na pia tabianchi na mazingira