IOM yasaidia kuwarejesha Ethiopia wahamiaji 100 Kutoka Yemen

30 Mei 2018

Raia 101 wa Ethiopia waliokuwa wahamiaji nchini Yemen wameondoka kwa hiyari kwa msaada wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM na kurejea nyumbani kupitia bandari ya Hudaydah.

Kwa mujibu wa IOM wahamiaji hao ambao hivi sasa wako safarini kupitia ghuba ya Aden hadi Djibouti kabla ya kuwasili nyumbani , wameondolewa kufuatia mapigano ambayo yamekaribia katika eneo la Hudaydah walikokuwa wakiishi.

IOM inawapa msaada wa usafiri hadi watakapowasili Ethiopia kwa ushirikiano na serikali ya Ethiopia na Yemen. Kundi hilo la kwanza lililoondoka linajumuisha wanawake 51 na watoto 33 ambao walijikuta wametelekezwa nchini Yemen. Ni kundi lisilojiweza kabisa miongoni mwa jumla ya wahamiaji 300  ambao IOM imeahidi kuwasafirisha hadi nyumbani endapo hali ya hewa ya bahari na usalama vitaruhusu.

Asilimia kubwa ya wahamiaji hao 300 wamekuwa wakishikiliwa katika kituo  cha serikali mjini Sana’a, ambako mkurugenzi wa operesheni na masuala ya dharura wa IOM Mohammed Abdiker, aliwatembelea mapema mwezi huu kutathimini hali yao.

Wahamiaji wengine wamekuwa wakihifadhiwa na familia za wasamaria wema na hivi sasa IOM inashirikiana na familia hizo kuwasaidia hadi pale watakaposafirishwa kwa hiyari yao kurejea nyumbani.  Miongoni mwa msaada wanaopewa na IOM ni pamoja na chakula, vifaa vya kujikimu, huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter