Changamoto bado zipo Libya lakini kuna matumaini: Salame

21 Mei 2018

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa ujumbe wa Umoja huo nchini Libya UNSMIL, Ghassan Salame amesema kuwa mapigano baado yanaendelea   katika mji wa Derna ulioko mashariki mwa taifa hilo.

Bwana Salame  amesema hayo leo akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani lililokutana kuangazia hali ya usalama na kibinadamu nchini humo.

Amesema mapigano katika mji huo wa Derna ni kati ya vikosi vitiifu vya Hafar dhidi ya makundi aliyoyaita ya kigaidi akisema mapigano hayo yanasababisha vifo vya raia pamoja  na uharibifu kubwa wa mali.

Amefafanua kuwa mapigano bado yako katika viunga vya mji huo na kuongeza kuwa wana wasiwasi endapo mapigano yataingia katikati ya  mji huo hawajui litakalowapata raia wengi ambao bado wamekwama katika mji huo.

Mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amezihimiza pande zote husika kujizuia na kufanya kila liwezekanalo kulinda raia wa kawaida akisema,

“Umoja wa Mataifa umejizatiti kushughulikia suala la kibinadamu endapo mambo yataendelea kuwa mabaya zaidi na tunaomba pande zote zikubali  msaada wa kibinadamu na wa kiutibabu uingie katika sehemu za mapambano.”

Pia amesema kuwa mjini Tripoli kulitokea mashambulio ambapo watu 13 walipoteza maisha yao baada ya makao ya tume ya uchaguzi kushambuliwa na kundi la ISIL ambalo baadaye lilijigamba kuhusika.

Amesema kuwa shambulio hilo lilijaribu kutibua  mchakato wa uchaguzi, lakini tume ilisimama kidete na kusisitiza utayari wake kusimamia uchaguzi.

Mbali na hayo amesema kuna mazuri yaliyotokea kama vile  uchaguzi wa kiongozi wa baraza kuu la kitaifa ,uliofanyika bila bughudha akiongeza kuwa “Katika mji wa Zawiya, ambao ni wa nne kwa ukubwa nchini Libya, na unapatikana umbali wa kilomita 40 magharibi mwa Tripoli, kulifanyika uchaguzi wa baraza la manispaa ya mji huo.”

Uchaguzi huo ulifanyika Mei 12 na ndio wa kwanza tangu mwaka wa 2015.

Bwana Salame amesema kuwa “La msingi kwa watu wa Libya ni serikali ya kitaifa ikubali  bajeti ya taifa ya mwaka 2018.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter