Umoja wa Mataifa walaani shambulizi la bomu mjini Benghazi Libya

10 Agosti 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kupitia ujumbe uliotolewa na msemaji wake jumamosi hii mjini New York Marekani, amelaani vikali shambulizi la bomu la kutegwa katika gari lililotokea mapema leo mjini Benghazi Libya ambapo  wafanyakazi watatu wa Umoja wa Mataifa wamepoteza maisha na wengine watatu kujeruhiwa.

Bwana  Guterres ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia za waliofariki na pia akawatakia kupona haraka wale wote waliojeruhiwa.

Aidha ametoa wito kwa mamlaka za Libya kufanya kila jitihada za kuwatambua waliohusika na kuwapeleka katika mikono ya sheria.

Katibu Mkuu Guterres pia ametoa wito, “pande zote ziheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano wakati wamaadhimisho ya Eid al-Adha na kurejea kwenye meza ya mazungumzo kutafuta mstakabali wa wanaoustahili watu wa Libya.”

Awali Umoja wa Mataifa ulikuwa umetoa wito wa kuwepo usitishaji mapigano na pia kuwaruhusu mahujaji kurejea nyumbani salama ili kuwaruhusu watu kuadhimisha na kusherekea sikukuu ya kidini ya Eid al adha lakini ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL ulikuwa umetoa taarifa ikieleza kuwa ni upande mmoja tu ambao ulikuwa umeleta majibu ya kuheshimu wito wa usitishaji mapigano hukuupande wa LNA yaani Libyan National Army ukikaa kimya.

Baraza la usalama laijadili Libya katika kikao cha dharura

Wakati huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo jumamosi limekaa na kuijadili Libya katika  kikao cha dharura kilichoitishwa na Poland na Ufaransa.

Katika kikao  hicho kilichoanza na dakika moja ya utulivu wa maombolezo, rais wa sasa wa Baraza hilo ambaye pia ni mwakilishi wa kudumu wa Poland katika Umoja wa Mataifa, Joanna Wroneka amesema,  “hao wafanyakazi mashuja walikuwa wanafanya kazi kwa mamlaka yanayotolewa na Baraza hili ili kuhakikisha mstakabali salama wa watu wa Libya. Tunaenzi kujitolea kwao kwa mwisho katika kusaka amani."

Wajumbe wa kikao hicho wamelaani vikali shambulizi hilo na wakatuma salamu zao za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha huku wakiwatakia majeruhi kupona haraka.

Naye Bintou Keita ambaye ni msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika katika  masuala ya siasa na ujenzi wa amani akizungumza katika kikao hicho amesema, "shambulio hilo baya limetokea wakati wakazi wa Benghazi wakijiandaa na sikukuu ya Eid al-Adha katika eneo linalodaiwa kuwa chini ya mamlaka ya vikosi vya jeshi la kitaifa la Haftar. Hii inaonesha hali ya hatari ya ugaidi kote nchini Libya na mipaka ya udhibiti wa usalama wa kukosekana kwa serikali na jeshi na polisi wa kufanya kazi kote nchini."

Keita amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa hauna mpango wa kuondoka nchini Libya, "katika siku za hivi karibuni na nafasi yetu inasalia na watu wa Libya kama wenzetu mashujaa ambao wamejitolea maisha yao leo kwa ajili ya watu wa Libya."

UN Photo/Evan Schneider
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likisimama katika dakika moja ya ukimya katika kikao chake cha dharura kilichoitishwa baada ya mlipuko wa bomu mjini Benghazi Libya na kuwaua wafanyakazi watatu wa Umoja wa Mataifa.

 

Kuhusu usitishaji mapigano

Aidha msaidizi huyo wa Katibu Mkuu, amelifahamisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa vikosi vya jeshi la kitaifa chini ya kamanda Haftar na  upande wa Waziri Mkuu Serraj wamekubaliana na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, kusitisha mapigano katika kipindi hiki cha kuadhimisha na kusherehekea sikukuu, hatua hii ikianzwa kutekelezwa usiku wa leo.

"Nina matumaini kuwa pande zote mbili kwa hakika zitatekeleza makubaliano. Vurugu zisizo na maana na faida zinatakiwa kukoma. Tumeweka wazi, katika matukio kadhaa, mbele ya hadhara hii hii kuwa hakuna upande utakaoibuka mshindi wa mgogoro huu. Leo ni ushahidi wa wazi kuwa kuna walioshindwa wengi, ambao wengi wao ni wananchi wasio na hatia." Amesisisita Bi Keita.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud