Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilichokishuhudia Sudan Kusini kinasikitisha:Lowcock

Amani ya kudumu nchini Sudan Kusini ni muarobaini kwa mustakhbali wa watoto kama hawa nchini humo ambao sasa haki zao za msingi zinasiginwa.
UNMISS
Amani ya kudumu nchini Sudan Kusini ni muarobaini kwa mustakhbali wa watoto kama hawa nchini humo ambao sasa haki zao za msingi zinasiginwa.

Nilichokishuhudia Sudan Kusini kinasikitisha:Lowcock

Amani na Usalama

Nilichokishuhudia Sudan Kusini kwa maelfu ya watu waliotawanywa kinasikitisha, amesema msaidizi wa Katibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu Mark Lowcock ambaye leo anahitimisha ziara ya siku mbili nchini humo.

(Taarifa ya Grace)

Lowcock ambaye yuko Sudan Kusini ili kushuhudia hali halisi na changamoto zinazoikabili jamii na wahudumu wa misaada wanaohatarisha maisha yao kila siku ili kuwasaidia waathirika wa machafuko nchini humo amesema kwa hakika hali si shwari

(SAUTI YA MARK LOWCOK)

“Hali ni ngumu sana, ni mfano mdogo tu wa changamoto nyingi zinazotukabili hapa sudan kusini kama mashirika ya kibinadamu. Watu wako hapa sio kwa sababu wanataka kuwa hapa , ni kwa sababu wanataka kuwa salama.,Nimeona mabango waliyonibebea watoto nilipofika , wanachokitaka ni Amani na elimu na ndicho watu wanachokitaka kila mahali.”

Lowcock ametembelea makazi ya ulinzi wa raia kwenye kituo cha Umoja wa Mataifa na kukutana na baadhi ya wakimbizi wa ndani waliotawanywa na vita vinavyoendelea, na pia leo amekuwa katika eneo la Kusini mwa nchi hilo ambalo ni hatari zaidi kwa wahudumu wa misaada.

Takribani theluthi moja ya watu wote sudan Kusini wametawanywa na milioni 1.8 ni wakimbizi wa ndani na wengine milioni 2.5 wamesaka hifadhi nchi jirani na hali ni mbaya sana.

Lowcok amekutana pia na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan kusini UNMISS David Shearer kujadili suluhu ya kisiasa na hali ya usalama , lakini pia machafuko ya karibuni katika jimbo la Unity na bwana Shearer akamweleza

(SAUTI YA DAVID SHEARER)

Walinda amani wetu wamekuwa nje kila wawezapo ili kurejesha utulivu na kujiamini katika eneo hilo , lakini licha ya hivyo tunachokishuhudia hapa kinatisha, kuna vibanda na nyumba zinachomwa moto, wanawake wanabakwa, watoto wanauawa. Nilimuona mtoto ambaye amepigwa risasi kwa macho yangu nilipokuwa hapo siku chache zilizopita na watu wanaogopa sana.”

Ameongeza kuwa hivi sasa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada wanajitahidi kuwapa hifadhi wanaosaka pa kujificha.