Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauritania mwachilieni mara moja mwandishi wa blog:UN

Picha: UNESCO
Uhuru wa kutumia mitandao.

Mauritania mwachilieni mara moja mwandishi wa blog:UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kundi la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wameelezea hofu yao kuhusu kuendelea kushikiliwa rumande kwa mwandishi wa blogu wa Mauritania Cheikh Ould Mohamed M’kheitir kwa mdai ya kukiuka haki za binadamu.

Bwana M'kheitir anasalia korokoroni serikali ikidai ni kwa usalama wake licha ya kustahili kuachiliwa kutokana na muda ambao tayari ameshatumikia kizuizini.

Hofu ya wataalamu hao wa haki za binadamu ni kwamba, mazingira ya rumande yameathiri afya yake kwa kiasi kikubwa na wanasema wamekuwa wakiwasilina na serikali ya Mauritania mara kadhaa wakiitaka kumwachilia huru mwandishi huyo na kumuhakikishia usalama wake kwani amekuwa rumande sasa kwa miaka minne.

Wameongeza kuwa mashitaka dhidi yake na hukumu ya kifo aliyopewa awali kwa kutekeleza haki ya msingi ya kujieleza, kwa hakika inakiuka sharia za kimataifa za haki za binadamu na mikataba ya kimataifa ambayo Mauritania imeiridhia. Bwana M’kheitir alikamatwa tarehe 2 Januari 2014 na alihukumiwa kifo kwa uasi Disemba 2014 baada ya kuchapisha makala kwenye blog yake ikihoji matumizi ya dini kuhalalisha ubaguzi wa kikabila .

Na tarehe 9 Novemba mwaka 2017 mahakama ya rufaa ya Nouadhibu ili futa hukumu yake ya kifo na kuibadili kuwa kifungo cha miaka miwili jela na kumtoza faini kwa kukashifu dini, hali ambayo inamruhusu kuachiliwa mara moja kutokana na muda ambao tayari ameshakaa jela.

Lakini siku iliyofuata mwendesha mashitaka mkuu alikata rufaa kupinga uamuazi huo na hadi sasa haijulikani endapo lini kesi hiyo itafikiriwa upya na mahakama kuu.