Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na AU waimarisha mkakati kulinda haki za binadamu

Luteni wa kwanza Sigit Jatmiko, mmoja wa askari wa umoja wa Mataifa kutoka Indonesia kwenye UNAMID anazungumza na watoto katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abu Shouk wakati wa ziara yake ya kupiga doria.
UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Luteni wa kwanza Sigit Jatmiko, mmoja wa askari wa umoja wa Mataifa kutoka Indonesia kwenye UNAMID anazungumza na watoto katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abu Shouk wakati wa ziara yake ya kupiga doria.

UN na AU waimarisha mkakati kulinda haki za binadamu

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika AU wamefikiana kuimarisha mikakati yao ya ushirika katika kuzuia na kushughulikia ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu barani Afrika kabla haujawa janga kubwa.

Akizungumza katika majadiliano ya ngazi ya juu kuhusu haki za binadamu kwenye Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia, Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema kazi ya AU kuhusu kutatua na kuzuia migogoro ni nguzo ya utulivu na usalama kwenye maeneo mengi yenye machafuko barani humo.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa haki za binadamu na mtazamo thabiti ambao unaepuka ukiukwaji dhidi ya raia utazifanya juhudi hizo kuwa na uzito mkubwa katika mipango ya muda mfupi na ya muda mrefu.

AU inataka kuimarisha utaalamu wake katika kufuatilia haki za binadamu, kutoa taarifa za ukiukwaji wa haki hizo na kuuzuia ukiukwaji huo.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inaweza kuipa AU uzoefu wake, mambo ya kujifunza na mipango mizuri ya kuzingatia ili kuisaidia kuyatumia mambo hayo katika muktada wa Afrika wakati ikihakikisha inakwenda sanjari na mfumo wa haki za binadamu wa kimataifa na kikanda.

Zeid pia amesema haki za binadamu na haki za kisheria ni muhimu katika ujenzi na udumishaji wa amani endelevu, kwani amani ya kudumu haiwezi kupatikana kwa kufanya mambo kama mazoea na kuwa na mtazamo unaoruhusu wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu kukwepa mkono wa sheria.

Pande hizo mbili, UN na AU wameafikiana pia kuendelea kufanya kazi pamoja ili kuanzisha mfumo wa haki za binadamu kwa ajili ya operesheni za amani za AU, kuanzisha na kutekeleza mkakati wa pamoja kuhusu haki za binadamu na uwajibikaji.

Washirika hao wamebaini kuwa ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana ni kikwazo kikubwa cha amani na maendeleo hivyo watashirikiana katika kuhakikisha watu wote wanapata fursa ya kufurahia haki zao na pia kuboresha taasisi za haki za binadamu barani Afrika hususan tume ya Afrika kuhusu haki za binadamu.