Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchafuzi wa hewa unatishia sisi sote-WHO

Huko Ulaanbaatar nchini Mongolia kiwango cha hewa chafukiko juu.
WHO/Yoshi Shimizu
Huko Ulaanbaatar nchini Mongolia kiwango cha hewa chafukiko juu.

Uchafuzi wa hewa unatishia sisi sote-WHO

Afya

Asilimia 90 ya wakazi wa dunia huvuta hewa chafu na hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la afya duniani, WHO  iliyotolewa leo.

Ripoti hiyo inasema uvutaji huo wa hewa hiyo umesababisha  zaidi ya milioni 7 kufariki dunia kila mwaka kutokana na chembechembe wanazopata wakivuta hewa chafu.

WHO inasema chembechembe  za hewa chafu zinapoingia katika mapafu au moyo huweza kusababisha magonjwa  kama vile moyo na pumu.

Ingawa mataifa mengi sasa yanachukua hatua dhidi ya hewa chafu, WHO inasema bado takwimu za vifo ni za juu.

Maria Neira ni mkurugenzi wa idara ya afya ya umma, mazingira na masuala ya kijamii wa WHO.

(SAUTI YA MARIA NEIRA)

Raia  9 kati ya 10  duniani wanavuta chembechembe hizo ambazo zinakwenda ndani ya mapafu yetu na kusababisha maradhi makubwa na kisha zinakwenda kwenye mfumo wa kusukuma damu pia. Na hilo linasababisha moja ya hatari kubwa za kimazingira kwa afya zetu na kuchangia vifo milioni 7 kila mwaka, Hali hii haikubaliki na ndio sababu WHO inazindua ripoti hii.

Akitoa kauli kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus, amesema uchafuzi wa hewa ni tishio kwa kila mtu lakini wanaoumia zaidi ni watu maskini.

Amesema haikubaliki kwamba watu billioni tatu na wote ni wanawake na watoto bado wanavuta hewa chafu kila siku inayotoka kwenye majiko wanayotumia majumbani.

Dkt. Ghebreyesus [GeBreYeSus] ameonya kuwa ikiwa hakutachukuliwa hatua za haraka, kamwe dunia haitaweza kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya kuhakikisha kila mtu anavuta hewa safi.

Mkuu huyo wa WHO amesema ni matumaini yake kuwa viongozi mbalimbali wakiwemo mameya wa miji watachukua hatua madhubuti.

Amepongeza serikali ambazo amesema zimeanza kuvalia njuga suala hilo kwa kuweka njia za kupunguza utoaji wa hewa chafu katika maeneo yao.