Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania, Kenya kidedea katika kusambaza umeme- Ripoti

Programu ya kufanikisha nguvu za umeme vijijini nchini Tanzania. Picha: World Bank

Tanzania, Kenya kidedea katika kusambaza umeme- Ripoti

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Dunia haiku katika mwelekeo wa kutimiza malengo yaliyowekwa ya kuwa na nishati salama na endelevu ifikapo mwaka 2030, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika matano ya kimataifa yanayohusu nishati.

Ripoti inasema ingawa kuna mafanikio katika baadhi ya sekta, kwa ujumla mwelekeo unakatisha tamaa.

Mathalani ripoti hiyo iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia, inataja mafanikio ya kupanuliwa kwa huduma za umeme katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, Kenya na Ethiopia.

Hata hivyo ripoti inasema matumizi ya nishati endelevu hayajapatiwa kipaumbele katika sekta a usafirishaji na vipashajoto, maeneo ambayo huchangia asilimia 80 ya matumizi ya nishati duniani.

Ripoti inaweka bayana kuwa nishati ya jua imeanza kupata kipaumbele, ingawa bado imejikita katika maeneo machache.

Akizungumzia ripoti hiyo Mwakilishi wa Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu nishati endelevu, Rachel Kyte amesema takwimu hizi zinaonyesha kuwa hatua zaidi na utashi wa kisiasa vinahitajika ili kufikia ahadi ya kuhakikisha kila mtu ana nishati salama na endelevu ifikapo 2030.

Wametaka serikali ziwekeze katika teknolojia na mifumo ya biashara itakayorahisisha kila mtu kupata nishati salama ikiwemo umeme.