Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipomakinika Jodari watatoweka: UN

UN Photo/M Guthrie
Mvuvi anakagua samaki katika soko la Pusan nchini Korea.

Tusipomakinika Jodari watatoweka: UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Samaki Jodari au maarufu kama Tuna ni samaki wanaopendwa kwa sababu mbalimbali, kuanzia kutoa lishe bora hata kutumiwa katika kuburudisha mashuleni, lakini sasa wako katika hatari kubwa ya kutokuwa endelevu na kuweka mustakhbali wao njia panda umesema leo Umoja wa Mataifa.

Katika maadhimisho ya pili ya siku ya Jodari duniani ambayo kila mwaka hua Mei pili Umoja wa Mataifa unasema , kutokana  na umuhimu wa Jodari kiuchumi na kuwa chanzo kikubwa cha lishe bora kwa nchi zote zinazoendelea na zilizoendelea katika nchi zinazopitiwa na bahari ya Indi, Atlantic, Pacific na Mediterranean, matokeo yake mahitaji ya samaki hao yameongezeka na kuweka mustakhbali wao katika tishio kubwa.

Jodari hao ambao wamegawanyika katika aina 40 tofauti wanatumiwa zaidi katika uzalishaji wa bidhaa mbili, moja jorari za makopo na pili mlo aina ya sushi.

Na kwa kuwa samaki Jodari wanaingiza asilimia 20 ya thamani ya samaki wote wanaovuliwa baharini na kuchangia zaidi ya asilimia 8 ya biashara ya kimataifa ya samaki, katika maadhimisho ya leo Umoja wa Mataifa unasema ni hatua muhimu sana ya kutambua jukumu kubwa la samaki Jodari  katika maendeleo endelevu, uhakika wa chakula, fursa za kiuchumi, na maisha ya watu kote ulimwenguni na hivyo kuhakikisha uvuvi wa samaki hao unakuwa endelevu ili wasitoweke.