Kulikoni maendeleo yafukuzishe watu wa asili kwenye makazi yao?

16 Aprili 2018

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák amefungua jukwaa la watu wa jamii ya asili akisema katu isisahaulike kuwa Umoja wa Mataifa ni kwa ajili ya watu wote ikiwemo watu wa asili.

Amewaambia wajumbe kuwa ingawa kuna mafanikio yamepatikana katika kujumuisha kundi hilo bado juhudi zinatakiwa ikiwemo kuwanasua katika lindi la umaskini.

Amesema asilimia 15 ya watu wote maskini duniani ni watu wa jamii ya asili kwa hiyo amesema.

(Sauti ya Miroslav Lajčák )

“Hiyo inashtua. Na umaskini siyo changamoto pekee inayowakabili. Haki zao zinakiukwa. Mara nyingi hawana makazi na shule zenye staha. Wanatengwa na kuenguliwa kwenye mifumo inayopaswa kuwalinda. Wanakabiliwa na ghasia na hata vifo pindi wanapotetea haki zao.”

Akagusia pia moja ya mada kuu ya jukwaa hilo ambayo ni umiliki wa ardhi kwa watu wa asili akisema watu wa asili wanafukuzwa kwenye maeneo ambayo mababu zao waliotangulia waliyatambua kuwa ni nyumbani.

Kwa mantiki hiyo akanukuu wito uliotolewa na mwanaharakati mmoja wa maji wakati wa mkutano wa maji ulioandaliwa na Rais huyo wa Baraza Kuu akisema..

(Sauti ya Miroslav Lajčák )

“Hatuwezi kuendelea kujadili ardhi ya watu wa asili kama vile ni sawa na maeneo mengine. Tunapaswa kufahamu vyema umuhimu wa ardhi hizo kwa jamii zao. Ardhi hizo zinawakilisha maisha yao, imani zao, familia na zaidi ya yote uhai. Kwa hiyo nafurahi tunajikita kwenye masuala haya kwenye jukwaa hili la 17.”

Mkutano huo wa wiki mbili utakuwa ni mjadala wa wazi kwa wiki ya kwanza na wiki ijayo itakuwa na vikao vya faragha.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter