Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mifumo ya elimu ya lugha tofauti ni muarobaini wa kutunza lugha za asili- Bi. Mohammed

Jamii ya wamasai imeendelea kuhifadhi si tu lugha yake bali pia tamaduni, ingawa mabadiliko ya maisha yanatishia tamaduni na mila.
ILO/Marcel Crozet
Jamii ya wamasai imeendelea kuhifadhi si tu lugha yake bali pia tamaduni, ingawa mabadiliko ya maisha yanatishia tamaduni na mila.

Mifumo ya elimu ya lugha tofauti ni muarobaini wa kutunza lugha za asili- Bi. Mohammed

Utamaduni na Elimu

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani hii leo Naibu Katibu Mkuu wa chombo hicho Amina J. Mohammed ameongoza tukio la maadhimisho ya siku ya watu wa asili, ambayo maudhui yalikuwa lugha za asili.
 

Akihutubia washiriki, Bi.Mohammed amesema, “tunapaswa kukumbuka na kuangazia watu wa asili waliopo maeneo mbalimbali duniani na ambao haki zao bado zinabinywa.”

Amegusia mifumo kandamizi iliyowekwa dhidi ya watu hao ambapo wanabaguliwa, na mbinu zao za maisha, tamaduni na utambulisho vinakandamizwa.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu hivi sasa duniani kuna watu wa asili milioni 370 waliosambaa katika mataifa 90, ikiwa idadi yao yote ni sawa na asilimia 5 ya wakazi wote duniani.

 

“Lakini wao ni miongoni mwa asilimia 15 ya watu maskini zaidi duniani. Lakini hivi sasa watu wa asili wanapaza sauti zao katika kona mbalimbali wakitaka wawe na mbinu endelevu za kujipatia kipato na kuishi, wakitetea bayonuai ambayo ni msingi wa maisha yao huku wakipaza sauti za uharibifu wa mazingira unaochochea mabadiliko ya tabianchi,” amesema Naibu Katibu Mkuu.

Watu wa asili wanatumia lugha zao kupaza sauti zao na madhila wanayokumbana nayo na ndio maana Naibu Katibu Mkuu ametaka lugha hizo zilindwe na zihifadhiwe.

“Elimu itakuwa na dhima kuu ya kuhakikisha kuwa watu wa asili wanaweza kufurahia na kutunza tamaduni na utambulisho wao,” amesema Bi.Mohammed akiongeza kuwa “kushindwa kuweka mfumo wa elimu wenye matumizi ya lugha tofauti na tamaduni za muingiliano kutaweka hatarini watu wa jamii za asili na kutishia uwepo wao.”
TAGS: Watu wa asili, Amina J.Mohammed