Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbivu mbichi kuhusu shambulio la Salisbury wiki ijayo

Ahmet Üzümcü, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutokomeza silaha za kemikali, OPCW.
UN /Rick Bajornas
Ahmet Üzümcü, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutokomeza silaha za kemikali, OPCW.

Mbivu mbichi kuhusu shambulio la Salisbury wiki ijayo

Amani na Usalama

Sasa hatma ya sakata la kemikali ya sumu huko Salisbury, Uingereza, ni wiki ijayo, hata hivyo Uingereza ndio itaamua kuweka bayana kilichobainika.

Matokeo ya uchunguzi kuhusu kinachodaiwa kuwa ni shambulio la kemikali dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi  pamoja na binti yake, lililofanyika nchini Uingereza yatapokelewa mapema wiki ijayo.

Hayo yamesemwa na  Mkurugenzi Mkuu wa  baraza tendaji la shirika linalozuia matumizi ya silaha za kemikali-OPCW, Ahmet Üzümcü wakati wa mjadala kuhusu sakata hilo huko The Hague, Uholanzi.

Bila kufafanua mengi Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea baada ya kuombwa na serikali ya Uingereza kufanya hivyo.

Amesema kile ambacho serikali ya Uingereza imeomba ni kutambua aina ya sumu inayodaiwa kutumiwa.

Ameongeza kuwa watalaamu wa OPCW walizuru maeneo mawili ya matukio ambako waathiriwa  wanasemekana walipewa sumu na kuchukua sampuli sio tu kutoka kwa wahusika lakini pia katika mazingira ya sehemu za tukio.

Hata hivyo amesema kuwa utaratibu wao hauruhusu kufichua majina ya wahusika katika uchunguzi huo na pia kutoa bayana aina ya sumu iliyogunduliwa.

Hata hivyo amesema sheria zinasema kuwa matokeo ya uchunguzi yanapatiwa yule aliyeomba kufanyika kwa uchunguzi na huyo ndiye anayeweza kufichua matokeo ya uchunguzi huo.

Nao Muungano wa Ulaya kupitia  kwa mwakilishi wa Bulgaria kwenye OPCW, Krassimir Kostov, umesema unakaribisha uchunguzi huo ulioitishwa na Uingereza na pia kusikitishwa na kile ulichoita hatihati ya Urusi ya kukataa kuitikia ombi la mwanzo la Uingereza la kuitaka iipatie taarifa kamili kuhusiana na sumu hiyo.