Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vuta nikuvute Barazani ni mwiba kwa wasyria

Jopo la wakaguzi na wachunguzi kutoka OPCW wakati wa ziara yao ya ukaguzi huko Damascus, Syria tarehe 1 Oktoba 2013
UN/Hend Abdel Ghany
Jopo la wakaguzi na wachunguzi kutoka OPCW wakati wa ziara yao ya ukaguzi huko Damascus, Syria tarehe 1 Oktoba 2013

Vuta nikuvute Barazani ni mwiba kwa wasyria

Amani na Usalama

Kama mliweza kuungana na kupitisha azimio kudhibiti silaha za kemikali nchini Syria, sasa mwashindwa nini kuendelea na umoja huo hadi silaha hizo zitokomezwe?  Ahoji Markram.

Shaka na shuku kuhusu matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria, vinalazimu kuwepo kwa mfumo madhubuti wa uchunguzi na uwajibishaji wahusika.

Thomas Markram, ambaye ni Mkurugenzi na Naibu Mwakilishi wa ngazi ya juu kuhusu udhibiti wa kuenea kwa silaha duniani, amesema hayo leo wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Baraza hilo lilikutana kujadili utekelezaji wa azimio lake namba 2118 la mwaka 2013 kuhusu utokomezaji wa silaha za kemikali nchini Syria ambapo Bwana Markram amesema ingawa jitihada zinaendelea za kuharibu maeneo mawili ya kuzalisha silaha za nyuklia Syria, bado kuna mkwamo.

Mathalani amesema jopo la kubaini ukweli kuhusu matumizi ya silaha hizo linaendelea na kazi yake hivi sasa huko Damascus, Syria..

Thomas Makram, ambaye ni Mkurugenzi na Naibu Mwakilishi wa ngazi ya juu kuhusu udhibiti wa kuenea kwa silaha duniani, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
UN /Manuel Elias
Thomas Makram, ambaye ni Mkurugenzi na Naibu Mwakilishi wa ngazi ya juu kuhusu udhibiti wa kuenea kwa silaha duniani, akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Thomas Markram)

“Ingawa hivyo, kama sote tunavyofahamu, hitimisho la jopo hilo halijumuishi vipengele kuhusu uwajibishaji kwenye visa ambamo kwavyo matumizi ya silaha za kemikali yamethibitishwa. Mfumo wa pamoja uchunguzi wa Umoja wa Mataifa na shirika la kutokomeza silaha za kemikali, OPCW ulianzishwa kwa lengo hili, lakini cha kusikitisha mamlaka yake hayakuongezwa baada ya kumalizika. Wakati tuhuma za matumizi ya silaha za kemikali hazijakoma kutolewa, uzingatiaji wa kuwepo kwa mfumo wa kuwajibisha umesuasua au umekoma kabisa.”

Na ndipo wajumbe wa Baraza hilo nao wakatoa maoni yao, mmoja wao ni Balozi Nikki Haley, mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Nikki Haley)

 “Tunarudi nyuma, kuelekea kwenye ulimwengu ambao tulidhani kuwa tumeshaachana nao. Tusipochukua hatua sasa na kubadili mwelekeo, hiyo ndio dunia itakayotufika haraka.”

Kutoka Uingereza ni mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Karen Pierce.

(Sauti ya Karen Pierce)

 “Hakupaswi kuwepo na wahanga wa mashambulizi ya silaha za kemikali. Iwe ni katika ukanda wa vita huko Syria au kwenye miji ya pembezoni huko Uingereza.”

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
UN/Eskinder Debebe
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vassily A. Nebenzia naye akafunguka.

(Sauti ya Vassily A. Nebenzia)

 “Sheria ya kimataifa inasambaratika pindi shuku na siyo ushahidi, inapogeuka kuwa malkia wa ushahidi. Hakuna uchunguzi au mfumo ambao unaitishwa sasa, hata hivyo nchi kadhaa zinaendelea kujinasibu kuwa silaha za kemikali zinatumika Damascus.”

Na ndipo Mounzer Mounzer, ambaye ni Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa akatanabaisha.

(Sauti ya Mounzer Mounzer)

 “Kinachosikitisha ni msisitizo kutoka baadhi ya serikali wa kujiteua wenyewe kuwa wasimamizi wa hatma ya watu na walinzi wa sheria ilhali historia yao ya kisiasa na ukoloni vinaashiria ukiukwaji wao wa mara kwa mara wa haki za watu hao.”

Ni katika kikao hicho ambapo Bwana Makram amerejelea wito wake wa kutaka umoja ndani ya Baraza la Usalama, umoja ambao amesema ulifanikisha kupitishwa kwa azimio namba 2118 na hivyo amesema umoja huo uwepo tena ili kuhakikisha kuwa matumizi ya silaha za kemikali Syria yanakoma na wahusika wanawajibishwa.