Wahamiaji watarajie nini kutoka Brussels?

4 Aprili 2018

Kila uchao manyanyaso wapatayo wahamiaji  yanaripotiwa kila kona ya dunia, na sasa Umoja wa Mataifa pamoja na Muungano wa Ulaya wameamua kuchukua hatua.

Huko Brussels, Ubelgiji hii leo viongozi waandamizi wa shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM pamoja na Muungano wa Ulaya wanajadili mustakhbali wa uhamiaji wakati huu ambapo kundi hilo linakabiliwa na sintofahamu. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta Massoi)

Sintofahamu hiyo ni pamoja na masuala ya ulinzi kwa wahamiaji walio hatarini zaidi kama wanawake, watoto na wazee, usimamizi bora wa mienendeo ya wahamiaji pamoja na makubaliano ya kimataifa kuhusu uhamiaji.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa IOM William Lacy Swing amekaribisha kuendelea kwa mazungumzo ya kimkakati kati ya shirika lake na EU hususan wakati huu ambapo changamoto za uhamiaji na fursa zake zinaibua mijadala ya kisiasa na kushika nafasi ya juu katika ajenda za Ulaya na kimataifa.

Maboya haya yanayoleta wahamiaji ndio sasa yatumika kutengeneza mikoba ya mgongoni tena ya gharama ya juu
PICHA: IOM/Francesco Malavolta (maktaba)
Maboya haya yanayoleta wahamiaji ndio sasa yatumika kutengeneza mikoba ya mgongoni tena ya gharama ya juu

Amesema huu ni wakati muafaka wa kuwa kitu kimoja katika kuainisha sera ya uhamiaji kimataifa kwa kuwa hoja zinazogonga vichwa vya watu kuhusu uhamiaji zinamgusa kila mtu kuanzia nchi tajiri, maskini hadi wahamiaji wenyewe walio hatarini.

Bwana Swing amesema fursa hii ya kihistoria itatoa mwanya wa kujenga mfumo ambamo kwao watu wataweza kusafiri kwa usalama, kihalali na bila shinikizo huku haki zao za msingi zikilindwa.

Mkutano huu ni wa tano wa aina yake kati ya IOM na EU tangu kuanza kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya pande mbili hizo mwaka 2012.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter