Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindi cha radio kutumika kuelimisha jamii kuhusu uhamiaji holela nchini Nigeria

Piassa anafanya kazi katika karakana ya baba yake baada ya kupokea mafunzo kutoka kwa UNIDO. Wahamiaji wanapokuja wanaonekana kama wanapokonya kazi za wenyeji kama hizi
UNIDO
Piassa anafanya kazi katika karakana ya baba yake baada ya kupokea mafunzo kutoka kwa UNIDO. Wahamiaji wanapokuja wanaonekana kama wanapokonya kazi za wenyeji kama hizi

Kipindi cha radio kutumika kuelimisha jamii kuhusu uhamiaji holela nchini Nigeria

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa,  IOM limezindua kipindi cha Radio nchini na Nigeria kiitwacho Abroad Mata kwa lengo la kuelimisha  umma kuhusu madhara  ya uhamiaji holela na fursa za kuhama kwa kufuata kanuni.

Uzinduzi huo umefanyika mjini Benin katika jimbo la Edo ambapo Abroad Mata ina mfululizo wa vipindi 13 kikijumuisha mchezo wa redio, shuhuda kutoka kwa wahamiaji waliorejea nyumbani, jopo la waatalamu wakichambua suala hilo pamoja na wasikilizaji kupiga simu na kuuliza maswali au kutoa maoni.

Kipindi cha kwanza kilijumuisha mchezo wa radio uitwao Safiri Salama ukiwa na simulizi ya Patricia, msichana wa kutoka Nigeria ambaye alijaribu kufika Ulaya kupitia Libya.

Mkuu wa ofisi ndogo ya  IOM  mjini Lagos na meneja wa mardi huo unaoendeshwa kwa pamoja kati ya IOM na Muungano wa Ulaya, EU Abraham Tamrat amesema wazo la kuwa na kipind hicho ni kuweka bayana madhila ya safari za kupitia jangwa la Sahara hadi bahari ya Mediteranea.

“Kipindi hiki kitasaidia kufungua uelewa na kuendeleza uhusiano wa kijamii na pia kusaidia watu kukabiliana na unyanyapaa dhidi ya wahamiaji wanaorejea,” amesema Tamrat.

Abroad kitarushwa kinachoandaliwa kwa lugha ya Pijini na Yoruba kinarushwa katika majimbo la Edo, Delta, Oyo, Ogun, Imo na Lagos.

Jimbo la Edo lina asilimia 50 ya wahamiaji wanaorejea.

IOM inasema tangu mwezi Aprili mwaka 2017 imesaidia wahamiaji zaidi ya 10,283 wa Nigeria kurejea nyumbani kutoka Libya, Niger, Mali na maeneo mengine ya mpito, mpango ambao shirika hilo limetekeleza kwa ushirikiano na EU.

Halikadhalika zaidi ya wahamiaji 3600 waliorejea wamepatiwa stadi za biashara ili kusongesha maisha yao.