Mkiongeza muda wa MONUSCO zingatieni mambo 3- Zerrougui
Hali ya usalama si shwari huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambapo mapigano baina ya makabila bila kusahau operesheni za kijeshi dhidi ya vikundi vilivyojihami vimesababisha maelfu ya watu kukimbilia nchi jirani. Uchaguzi unakaribia huku muda wa MONUSCO ukitarajiwa kuongezwa.
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemorkasia ya Congo, DRC, Leila Zerrougui ametaja mambo ya kuzingatiwa wakati muda wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO utaongezwa.
Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, Bi. Zerrougui ametaja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuhakikisha “Ni jinsi gani mchakato wa kisiasa na uchaguzi unaweza kuungwa mkono kwa msingi wa makubaliano ya tarehe 31 disemba mwaka 2016. Pili jinsi gani hali ya usalama inaweza kuwa ya utulivu na usalama wa raia wa DRC uweze kupatiwa hakikisho," amesema mwakilishi huyo maaalum.

Bi. Zerrougui ambaye pia ni mkuu wa MONUSCO ameonya kuwa hali inaweza kuwa mbaya iwapo mambo hayo hayatazingatiwa, “Kushindwa kujenga Imani kwa kuhakikisha makubaliano ya tarehe 31 disemba yanatekelezwa kwa kina na kwa uaminifu, itakuwa ni mwanya wa kuongeza mvutano wa kisiasa na kuchochea hatari za kuibuka kwa ghasia ili kukidhi matakwa ya kisiasa, hususan kwa minajili ya kuanza upya na kuongezeka kwa shughuli za vikundi vilivyojihami," Alisema.
Mwakilishi huyo maalum amesema ni muhimu wadau wote wasake mbinu kuhakikisha kwamba uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwisho wa mwaka huu unakuwa wa amani na halali na hivyo kuwa njia ya kuchangia utulivu na amani siyo tu DRC bali pia kwenye ukanda mzima.
Muda wa MONUSCO unatarajiwa kumalizika tarehe 31 mwezi huu.