Abdullah kinara dhidi ya FGM nchini Sudan

Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.
UNICEF/Holt
Visu vya mangariba sasa vitasalia butu kwa kuwa watoto wa kike, wanawake na jamii zimefunguka macho juu ya madhara ya ukeketeaji au FGM.

Abdullah kinara dhidi ya FGM nchini Sudan

Wanawake

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake na watoto wa kike, FGM,  ambapo  Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la idadi ya watu unajinasibu juu ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa katika vita hivyo. 

Watoto hawa wa kike wakisema bila woga kuwa walikataa kukeketwa!

UNICEF na UNFPA wanasema kuwa ujasiri huo umewezekana kutokana na mikakati ya kujengea uwezo jamii ili itambue madhara ya FGM.

Hadi sasa zaidi ya watu milioni 31.5 wametangaza hadharani kuachana au kupinga kitendo hicho. Jamii nazo 21, 700 zimesimama kidete kupinga.

Miongoni mwao ni Abdullah Ali Abdullah mkazi wa El Obeid nchini Sudan, mwanaume ambaye kwa miaka 30 amebeba jukumu la kuelimisha hata maimamu wa dini ya Kiislamu kupiga vita FGM.

Abdullah alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa matatizo ya uzazi aliyobaini miongoni mwa wanawake waliojifungua kwenye kituo alichokuwa anafanya kazi yalisababishwa na ukeketaji.

Alienda mbali zaidi na kubaini kuwa ukeketaji si fundisho la dini ya kiislamu kama ilivyoaminika kwa wakazi wa eneo la Kordofan Kaskazini, nchini Sudan.

Abdullah alipata vikwazo sana kuelimisha wanajamii waachane na FGM na ndipo alijiunga na Wizara ya Elimu ya eneo hilo na kupitia elimu ya dini alielimisha maimamu na masheikh kuhusu madhara ya FGM.

Kundi hilo lilielewa na sasa Abdullah ni kinara wa kupiga vita FGM huko Sudan kwa ushirikiano na UNICEF, UNFPA na wadau wengine.