Kikosi cha Burundi cha kulinda amani chawasili Somalia

22 Agosti 2017

Kikosi kipya cha ulinzi wa amani kutoka nchini Burundi BNDF, kimewasili nchini Somalia kwa ajili ya kazi hiyo itakayodumu kwa mwaka mmoja chini ya ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia AMISOM.

Kwa mujibu wa wavuti wa AMISOM, BNDF, chenye maafisa 45, kinachukua nafasi ya kikosi kingine cha 39 ambacho kimemaliza muda wake ambapo kimetimiza wajibu wa kusaidia ujumbe huo kuimarisha amani nchini Somalia.

Akizungumza baada ya kuwasili mji mkuu Mogadishu, Luteni Kapteni Philbert Hatungimana anaeyongoza kikosi cha Burundi, amesema matarajio ni kuwasaidia watu wa Somalia kurejelea amani.

Burundi ni nchi ya pili kupeleka vikosi vya kulinda amani nchini Somalia, baada ya Uganda. Nchi nyingine zinazochangia askari ni Kenya, Ethiopia na Djibouti.