Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado kuna mapungufu makubwa katika kukabiliana na haki za binadamu Guinea: UM

Bado kuna mapungufu makubwa katika kukabiliana na haki za binadamu Guinea: UM

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Andrew Gilmour akizungumza kwenye kikao cha haki za binadamu katika mjadala kuhusu Guinea, amesema licha ya ahadi ya serikali baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya mwisho ya mashauriano ya kitaifa ya Juni 29 kuweka kipaumbele katika mapambano dhidi ya uonevu, bado kuna mapungufu makubwa katika kukabiliana na matukio mengi.

Taarifa za ofisi yake zinasema bado kuna ukosefu wa uaminifu wa wananchi katika mfumo wa sheria, na hawajakabiliana na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu yanahusiana na matukio Septemba 28, 2009 ambapo inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 150 waliuawa na zaidi ya wanawake 100 walibakwa.

Pia watu wanawekwa kizuizini kwa muda mrefu kabla ya kesi kusikilizwa, kuna ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ukeketaji wa wanawake, na wahusika kutofikishwa mbele ya mahakama.

Bwana Gilmour amesema kuwa anatiwa moyo na matamshi ya serikali kwamba sasa wahusika watafikishwa mahakama mwaka huu lakini ameongeza kuwa ni ni muhimu wale walioshitakiwa kusimamishwa kazi za umma, ikiwa ni pamoja Gavana wa mji mkuu wa Conakry.

Gilmour ameongeza kuwa Guinea inapaswa kusaidiwa na jumuiya ya kimataifa ili kuhakikisha kwamba kesi hiyo ya kihistoria inafanyika kama ilivyopangwa mwaka huu.