Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wasaka hifadhi 15,500 wapata usajili wa awali Ugiriki

Zaidi ya wasaka hifadhi 15,500 wapata usajili wa awali Ugiriki

Nchini Ugiriki zaidi ya wasaka hifadhi 15,5000 wamefanyiwa usajili wa awali na hivyo kupatiwa kadi maalum wakati wakisubiri hatma yao ya kupata hifadhi ya kudumu barani Ulaya.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesaidia kazi hiyo iliyoanza tarehe Nane mwezi uliopita ambapo baada ya kupata kadi, wasaka hifadhi hao wana haki ya kupata huduma za msingi kwa mwaka mmoja

Msemaji wa UNHCR William Spindler amesema walengwa wa usajili huo ni wale wote waliokuwa wameingia Ugiriki kuanzia tarehe Mosi Januari mwaka 2015 hadi tarehe 20 Machi 2016 na kwamba..

(Sauti ya Spindler)

“Shughuli hii inalenga kubaini wale wenye haki ya kuungana na familia zao au kuhamishiwa nchi nyingine ya Muungano wa Ulaya. Halikadhalika itabaini watu wenye mahitaji maalum ili waweze kuelekezwa kwenye mashirika stahili na wapate misaada.”

Usajili huo wa awali unatarajiwa kukamilika mwanzoni au katikati mwa mwezi Agosti.