Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wateua atakayetetea haki za wapenzi wa jinsia moja

Umoja wa Mataifa wateua atakayetetea haki za wapenzi wa jinsia moja

Baraza la Haki za Binadamu, leo limeamua kumteua mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili na ubaguzi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja na watu wanaojitambua kwa jinsia tofauti na maumbile (LGBT).

Uamuzi huo umefikiwa baada ya mjadala uliohitimishwa baada ya rasimu ya azimio la kufanya uteuzi huo kufanyiwa marekebisho mara 11, likiungwa mkono na nchi wanachama 23, huku wanachama 18 wakilipinga. Wanachama sita hawakuonyesha kuegemea upande wowote.

Moja ya nchi zilizopendekeza azimio hilo ni Chile, na Mwakilishi wake wa Kudumu kwenye Umoja wa Mataifa huko Geneva Uswisi, Balozi Marta Mauras, ameileza Redio ya Umoja wa Mataifa ni kwa nini azimio hilo ni muhimu sana.

(Sauti ya Balozi Marta Mauras)

“Hii ni siku ya kihistoria kwa jamii ya kimataifa, na kwetu sote tunaoamini katika mfumo wa maoni ya wengi. Kwa sababu imedhihirishwa tena kuwa tunaweza kuketi chini na kukinzana, lakini tukaweza kukubaliana kwa njia ambayo itatimiza mahitaji ya angalau baadhi ya wanachama wa jamii ya kimataifa."

Naye Bwana Charles Radcliffe, Mkuu wa masuala ya kimataifa na ushirikiano kati ya serikali katika Ofisi ya Haki za Binadamu jijini New York, amesema hili ni tukio lenye umuhimu mkubwa.

Inamaanisha kuwa, kwa mara ya kwanza hapa kwenye Umoja wa Mataifa, Baraza la Haki za Binadamu limemteua mchunguzi atakayesafiri kote duniani na kuripoti kuhusu hali ya haki za binadamu za wapenzi wa jinsia moja na watu wanaojitambua na jinsia tofauti na maumbile yao.”

Amesema inatia furaha kwamba suala hili sasa litawekwa kwenye mfumo wa Umoja wa Mataifa kitaasisi hivi

"Tuna wataalam kuhusu masuala mengine, walioteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu, mathalan masuala ya ulemavu, au ubaguzi wa rangi, haki za wazee – na wamechangia pakubwa katika kuzifanya nchi wanachama kuyamulika masuala haya. Hatujawa na mtu yeyote kuhusu suala hili, na limekuwa pengo ambalo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu amekuwa akiweka wazi kwa kipindi kirefu sasa.”