Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KIfo cha Jo Cox ni kumbusho la kusimamia mitazamo inayotuunganisha:Eliasson

KIfo cha Jo Cox ni kumbusho la kusimamia mitazamo inayotuunganisha:Eliasson

Kifo cha mbunge wa Uingereza Jo Cox kilichotokea siku chache zilizopita ni kumbusho tosha la kusimamia maadili na misingi inayotuunganisha na sio kutugawanya, katika dunia ya leo iliyoghubikwa na changamoto nyingi.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Jan Eliasson, akizungumza kwenye hafla maalumu kwenye Umoja wa Mataifa hii leo, ya kuenzi maisha ya mbunge huyo aliyeuawa kwa kuchomwa kisu na kupigwa risasi.

Bwana Eliasson amesema kifo hicho ni mshituko mkubwa, na hasa jinsi kilivyotokea kikatili kwa mtu ambaye tabasamu lake, upendo wake na msimamo wake ulikuwa ni wa kuwaunganisha watu kwa upendo na sio kwa chuki. Ameongeza kuwa Jo alikuwa mtu wa watu, mwenye utu, alityeheshimu binadamu wote, na utu wake ulidhihirika kwa kila alichokuwa anakifanya.

Akinukuu maneno ya Jo “kuna mengi ya kutuunganisha kuliko kutugawanya” amesema ni kauli inayozunguka kote duniani kwa sasa sanjari na kauli ya mumewe, Brendan Cox: “chuki haina Imani, rangi wala dini, ni sumu kali”.

Eliasson ameongeza kuwa katika wakati huu wa majonzi na simanzi ni lazima kujiuliza nini tunaweza kufanya ili kumuenzi vyema Jo Cox na maisha yake. Na kuendeleza mapambano na misingi aliyoisimamia ya kuunganisha watu na sio kuwatenga.