Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na China waafiki kuongeza ushirikiano wa masuala ya anga:UNOOSA

UM na China waafiki kuongeza ushirikiano wa masuala ya anga:UNOOSA

Ofisi ya Umoja wa mataifa inayohusika na masuala ya anga za mbali (UNOOSA) na shirika la masuala ya anga la serikali ya Uchina (CMSA) wameafikiana kufanya kazi pamoja ili kuunda uwezo wa masuala ya anga kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kufuatia kutiwa saini makubaliano na ufadhili wa suala hilo mapema mwaka huu Wu Ping, naibu mkurugenzi mkuu wa CMSA, amewasilisha mradi huo katika kikao cha 59 cha kamati ya matumizi ya amani ya anga za mbali kwenye Umoja wa Mataifa mjini Vienna mapema wiki hii.

Chini ya makubaliano hayo, UNOOSA na CMSA watashirikiana kuwawezesha nchi wanachama wa Umoja wa mataifa , hususani mataifa yanayoendelea , kufanya majaribio ya anga ndani ya kituo cha anga cha Uchina, pia kutoa fursa za safari za ndege kwa wanaanga na wahandishi wa masuala ya anga.

Pande zote mbili pia zitachagiza ushirikiano wa kimataifa na masuala ya wannaanga na anga za mbali, pia kuelimisha kuhusu faida za teknolojia ya masuala ya anga, jinsi zinavyotumika na uwezo wa shughuli za teknolojia ya anga. CMSA itatoa fedha kusaidia UNOOSA katika suala hili.