Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwendesha mashtaka Bensouda achoshwa na dharau dhidi ya ICC

Mwendesha mashtaka Bensouda achoshwa na dharau dhidi ya ICC

Baraza la Usalama leo limekutana kujadili mwelekeo wa kesi dhidi ya Sudan iliyopelekwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusu uhalifu uliofanyika kwenye eneo la Darfur, nchini Sudan.

Akihutubia mkutano huo, Mwendesha Mshtaka wa ICC Fatou Bensouda amesema hali ya usalama kwenye eneo la Darfur bado ni tete. Amesema zaidi ya watu 120,000 wamelazimika kuhama makwao tangu mwanzo wa mwaka 2016, huku vifo vya raia 400 vikiripotiwa na kesi zaidi ya 100 za uhalifu wa kingono. Ameongeza kuwa ripoti zinaonyesha kwamba serikali ya Sudan imetekeleza kiasi kikubwa cha uhalifu huo.

Bi Bensouda amesema kwamba zaidi ya miaka kumi tangu kupelekwa kwa kesi hiyo mbele ya ICC, bado uhalifu unaendelea kutekelezwa na watu kuteseka kwa kiwango kikubwa.

Amesikitishwa na serikali ya Sudan ambayo inadharau wazi maazimio ya Baraza la Usalama na inashindwa kutimiza wajibu wake, huku Baraza hilo likikaa kimya kuhusu tabia hiyo.

Ameongeza kuwa ukimya huo umesababisha nchi nyingi wanachama wa ICC na wasio wanachama kualika na kupokea rais wa Sudan Al Bashir licha ya vibali vya kumkamata vilivyotolewa na ICC.

Bi Bensouda amesema hiyo inaonyesha mfano mbaya kwa viongozi wengine wanaotarajia kutenda uhalifu kama huo.

Halikadhalika, mwendesha mashtaka huyo ameeleza kuchoshwa na baadhi ya viongozi wanaojivunia kupuuza maazimio ya ICC, akisema tabia hizo ni ukiukaji wa wajibu wao chini ya mkataba wa Roma.