Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwongozo wa kutathmini mlo shuleni wazinduliwa

Mwongozo wa kutathmini mlo shuleni wazinduliwa

Mwongozo mpya wa kutathmini mlo shuleni kimataifa umetolewa leo na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Benki ya Dunia na asasi ya ubia ya Chuo Kikuu cha Imperial College London (PCD).

Mwongozo huo wa kisasa umeundwa ili kusaidia katika kuimarisha uwekezaji katika huduma muhimu ya kutoa chakula kwa watoto shuleni.

Mwongozo huo ambao umetokana na uzoefu katika nchi 14, umetolewa kufuatia maombi ya serikali na wadau katika mikakati ya maendeleo, ya mwongozo kuhusu jinsi ya kutunga na kutekeleza programu endelevu za mlo shuleni kwa kiwango kikubwa, na ambazo zinaweza kukimu viwango vinavyokubaliwa kimataifa. Nchi zilizohusika katika utafiti huo ni Botswana, Brazil, Cabo Verde, Chile, Cote D’Ivoire, Ecuador, Ghana, India, Kenya, Mali, Mexico, Namibia, Nigeria na Afrika Kusini.

Mwongozo huo una nyaraka zinazotathmini programu kadhaa za serikali za mlo shuleni, kwa minajili ya kutoa elimu, ushahidi na stadi bora za utendaji kazi kwa wanaofanya uamuzi na wanataaluma, katika kuimarisha juhudi za utoaji chakula shuleni.