Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CAR imeonyesha mfano kwa Afrika: Baraza la Usalama

CAR imeonyesha mfano kwa Afrika: Baraza la Usalama

Leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili hali ya usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na juhudi za Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSCA.

Mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa Amani kwenye Umoja wa Mataifa, Hervé Ladsous, amesema kuapishwa kwa rais mpya Faustin Archange Touadéra ni ishara ya kufanikiwa kwa mchakato wa mpito.

Amesema kinachomfurahisha zaidi ni kwamba rais huyo amezingatia kuheshimu katiba mpya na hasa udhibiti wa idadi ya mihula ya uraisi.

(Sauti ya Bwana Ladsous)

"Kwenye sehemu hii ya dunia, hakuna mifano mingi ya uchaguzi wa rais ambapo matokeo hayajulikani kabla ya tukio, hakuna mifano mingi ya uchaguzi bila vurugu, nadhani CAR imeonyesha mfano mzuri kupitia mchakato huo."

Hata hivyo Bwana Ladsous ameeleza kwamba hatua inayoanza sasa inakumbwa na changamoto zikiwemo kujisalimisha kwa waasi, kurudisha wakimbizi, kuboresha utawala wa sheria kwenye serikali za mitaa na kuleta maendeleo na huduma za kijamii kote nchini.