Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC kuelekea mkakati wa kimataifa dhidi ya madawa ya kulevya

UNODC kuelekea mkakati wa kimataifa dhidi ya madawa ya kulevya

Mkutano maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi ujao mjini New York, Marekani kuhusu tatizo la madawa ya kulevya duniani, utasaidia mamilioni ya wanawake, watoto na wanaume wanaokumbwa na tatizo hilo kote ulimwenguni.

Taarifa hiyo imetolewa leo na kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa huko Vienna Austria mwishoni mwa kikao cha 59 cha Kamisheni ya madawa ya kulevya kilichohudhuriwa na zaidi ya wawakilishi 1,500.

Awali akihutubia kikao hicho mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na madawa ya kulevya na uhalifu UNODC,Yury Fedeotov amepongeza juhudi za wawakilishi wa nchi wanachama walioafikiana kwenye mkutano huo, akisema ni hatua muhimu katika kufikia mkakati wa kimataifa wa kupambana na madawa ya kulevya.

Miongoni mwa maazimio yaliyopitishwa ni pamoja na mikakati mbadala kwa wakulima wa madawa ya kulevya, masuala ya afya na ustawi wa jamii, usawa wa jinsia kwenye miradi hiyo na viwango vya kimataifa kuhusu namna ya kutibu wagonjwa wa madawa ya kulevya.