Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mifuko ya plastiki marufuku huko Lamu, Kenya kuanzia Aprili

Mifuko ya plastiki marufuku huko Lamu, Kenya kuanzia Aprili

Nchini Kenya, harakati za uhifadhi wa mazingira zinachukua kasi ambapo gavana wa kisiwa cha Lamu ameamua kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia mwezi Aprili.Taarifa kamili na Grace Kaneiya

(Taarifa ya Grace)

Akizungumza huko Sheha, Gavana Issa Timamy amesema mifuko ya plastiki imekuwa ikiharibu mfumo wa bayonuai na maisha ya viumbe vya baharini ikiwemo kasa.

Bwana Timamy amenukuliwa na mtandao wa Climateaction unaoungwa mkono na UNEP katika kuangazia mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, akisema kuwa sasa wanaandaa sheria kwani taka zitokanazo na plastiki pamoja na kuharibu mazingira zimekuwa chanzo cha vifo vya wanyama ikiwemo punda.

Amesema sheria mpya siyo tu zitasaidia kuboresha usafi bali pia afya za wakazi wa Lamu na ametoa wito kwa wadau kuibuka na mbinu za kuhuisha taka za plastiki.

Ametaka wakazi hao kuiga mfano wa Zanzibar huko Tanzania ambako amesema marufuku ya plastiki yanazuia hata wageni kuingia na bidhaa za aina hiyo.