Watalaam waiomba Canada ikabili ukatili dhidi ya wanawake kutoka jamii asilia
Wataalam wa Umoja wa Mataifa wameisihi serikali ya Canada kukabiliana na mizizi ya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake wa jamii za watu wa asili nchini humo.
Taarifa imetolewa leo na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, baada ya wataalam hawa kukutana na waziri watatu wa serikali ya Canada waliopewa jukumu la kuanzisha uchunguzi rasmi wa kitaifa kuhusu wanawake na wasichana 1,200 waliouawa au kutoweka katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Wamesema uchunguzi huo unapaswa kuwa jumuishi na kuangazia chanzo cha ukatili huo.
Canada ilikuwa inanyoshewa kidole na wataalam wa haki za binadamu kwa kushindwa kukabiliana na visa hivyo na kuheshimu haki za wanawake na wasichana kutoka jamii za watu wa asili.
Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa asili Victoria Tauli Corpuz amekarisha hatua hiyo iliyochukuliwa hivi karibuni na serikali ya Canada ya kutambua ukiukaji wa haki unaowakumba wanawake na wasichana wa jamii za watu wa asili.