Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango kabambe wa kimataifa wazinduliwa kutoa matumaini ya ajira bora kwa vijana:ILO

Mpango kabambe wa kimataifa wazinduliwa kutoa matumaini ya ajira bora kwa vijana:ILO

Wakati dunia ikiwa katikati ya mtafaruku wa matatizo ya ajira kwa vijana yanayoambatana na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira, kazi zisizo na hadhi na kazi zenye ujira mdogo, mfumo wa Umoja wa mataifa umezindua mpango kabambe wa kuzalisha ajira bora kwa vijana na kuwasaidia katika kipindi cha mpito cha kutoka shule hadi kazini.

Mpango huo “mradi wa kimataifa wa ajira bora kwa vijana” umezinduliwa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na mkurugenzi mkuu wa shirika la kazi duniani ILO Guy Ryder kwenye jukwaa la kila mwaka la Umoja wa mataifa la vijana.

Akiuelezea mpango Ryder amesema ni ushirikiano wa kipekee na serikali, mfumo wa Umoja wa mataifa, makampuni ya biashara, taasisi za elimu, mashirika ya vijana na makundi mengine katika kuchapuza hatua za kuanzisha fursa mpya za usawa wa ajira katika uchumi wa kimataifa m na kuwasaidia vijana kupata ujuzi unaohitajika kushindana katika soko la sasa la ajira.

Ryder amewachagiza vijana kujihusisha kikamilifu na kuwa mawakala wa mabadiliko , akisistiza kwamba sauti zao lazima zisikike ili kuwa na jamii endelevu, kukabiliana na hali ya kutokuwepo usawa na kufungua njia ya amani, maendeleo na mustakhbali bora kwa wote. Jukwaa hilo linalohudhuriwa na mawaziri zaidi ya 20 na vijana zaidi ya 500 litahitimishwa kesho Jumanne.