Skip to main content

Mswada wa ufuatiliaji Uingereza watishia uhuru wa kijieleza: UM

Mswada wa ufuatiliaji Uingereza watishia uhuru wa kijieleza: UM

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu wameonya kuwa muswada wa ufuatiliaji nchini Uingereza, unatishia uhuru wa kujieleza na kujumuika ndani na nje ya nchi hiyo.

Katika taarifa yao wataalamu hao David Kaye anayehusika na uhuru wa kujieleza, Maina Kiai wa uhuru wa kukusanyika na kujumuika na Michel Forst anayehusika na watetezi wa haki za binadamu wameonyesha kuguswa mno na vipengele katika muswada huo.

Rasimu ya muswada huo ambao kwa sasa unatathiminiwa na Jopo la pamoja la Bunge la Uingereza inalenga kuoanisha sheria tofauti kuhusu uchunguzi wa polisi na mamlaka zingine kuhusu jinsi ya kufuatilia washukiwa.

Watalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesema ukosefu wa uwazi katika muswada huo, utawezesha watu binafsi kufuatiliwa bila wao kujua, na kukandamiza kabisa uhuru wa kujieleza na harakati za asasi za kiraia kwa ujumla.

Wamesisitiza urekebishwe kabla ya kupitishwa ili uendane na vigezo na sheria ya kimataifa kuhusu haki za binadamu.