Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Papa Francis kukutana kwa faragha na mwakilishi wa UM wa usalama barabarani

Papa Francis kukutana kwa faragha na mwakilishi wa UM wa usalama barabarani

Papa Francis atampokea na kukutana naye kwa faragha alhamisi wiki hii mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu usalama barabarani, Jean Todt, atakayeambatana na Christian Friis Bach, katibu mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa ya uchumi kwa Ulaya.

Viongozi hao watajadili haja ya kuongeza usalama barabarani duniani kote ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu , ikiwa ni katika lengo la kupunguza kwa nusu vifo vitokanavyo na ajali za barabarani ifikapo mwaka 2020 kama ilivyoorodheshwa kwenye malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s).

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO kila mwaka watu milioni 1.25 hufariki dunia kutokana na ajali za barabarani, na hususani katika nchi za kipato cha chini na cha wastani na huku wengine milioni 20 hadi 50 wakijeruhiwa.

Ajali za barabarani ndio chanzo kikubwa cha vifo kwa vijana wa kati ya umri wa miaka 15-29 na hivi karibuni itakuwa ndio sababu inayoongoza kwa vifo vya watoto wa umri wa miaka 5-14.