Bwana Ban azungumzia mabadiliko ya tabianchi na Rais wa Malta

Bwana Ban azungumzia mabadiliko ya tabianchi na Rais wa Malta

Akiwa ziarani nchini Malta, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekutana naRais wa nchi hiyo  Marie Louise Coleiro Preca.

Kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Katibu Mkuu amekumbusha kwamba Malta imekuwa nchi ya kwanza kuzungumzia swala la mabadiliko ya tabianchi mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1988.

Bwana Ban na Bi Coleiro Preca wamejadiliana kuhusu maswala yanayohusiana na wakimbizi na wahamiaji, huku Katibu Mkuu akikaribisha ukarimu wa Malta na haja ya kuongeza mshikamano wa kimataifa ili kukabiliana na janga hilo.

Aidha viongozi hawa wawili wamezungumza kuhusu jinsi ya kupambana na itikadi kali na ugaidi, kukuza utamaduni wa amani na kutekeleza ajenda ya maendeleo endelevu. Wamekubaliana juu ya umuhimu wa kushirikisha vijana na watoto katika kujenga mustakabali bora kwa jamii na kutunza mazingira.