Skip to main content

Bado kuna fursa ya kuafikiana Burundi: Kamisheni

Bado kuna fursa ya kuafikiana Burundi: Kamisheni

Mwenyekiti wa mfumo wa kushughulikia amani Burundi ulio chini ya Kamisheni ya Ujenzi wa amani ya Umoja wa Mataifa, Jurg Lauber amependekeza kuwa Kamisheni hiyo isaidie Burundi katika kujengea uwezo wa Kamisheni ya Kitaifa ya Mazungumzo jumuishi, CNDI iliyoteuliwa mwezi uliopita.

Hii ni moja ya maoni aliyotoa mwenyekiti huyo leo akiwasilisha ripoti yake kuhusu ziara ya siku tatu aliyohitimisha nchini humo hivi karibuni.

Bwana Lauber pamoja na pendekezo hilo ameelezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kuzorota zaidi kwa hali ya usalama huku akisema kwamba ameshuhudia kiwango kikubwa cha ushawishi wa vijana kutoka pande zote za mzozo, zinazosambaza chuki kwenye jamii.

(sauti ya Lauber)

“ Ziara ya siku tatu kwenye mji mkuu wa Burundi , Bujumbura, haikuniwezesha kupata tahmini thabiti ya hali ya usalama. Nimehisi kiwango kikubwa cha mvutano na ukosefu wa uaminifu. Baada ya jioni, watu hawatembei tena barabarani, na baada ya saa nne za usiku kuna amri ya kutotembea . Vituo vya ukaguzi wa magari ni dalili ya hali ya ukosefu wa usalama. Lakini nimeshuhudia kwamba raia wanaendelea na shughuli zao za kila siku, ikionyesha kwamba wanajaribu kuvumilia licha ya hali ya wasiwasi na uoga."

 Kuhusu jitihada za kufikia suluhu ya kisiasa, amesema kwamba Kamisheni ya Kitaifa ya Mazungumzo, CNDI, iko tayari kusaidia ili kujengewa uwezo.

Akitaja ukosefu wa uaminifu baina ya Burundi na nchi jirani, amependekeza kuendeleza juhudi za kikanda za mchakato wa mazungumzo, kwa ushirikiano wa CNDI.

Bwana Lauber ameeleza kwamba anatarajia kurudi Burundi Mwezi Januari mwaka 2016.

Kwenye mjadala uliofuata ripoti hiyo, mjumbe wa uwakilishi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa amekariri wito wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kuunda serikali ya muungano wa kitaifa nchini Burundi.