Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani shambulio la bomu Nigeria

Ban alaani shambulio la bomu Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani shambulio la bomu mjini Yola nchini Nigeria, Kaskazini Mashariki mwa jimbo la Adamawa lililosababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Akiongea na waandishi wa habari mjini New York msemaji wa Katibu Mkuu Stéphane Dujarric, amesema Ban ametuma salaam za rambirambi kwa familia za waathiriwa, serikali na watu wa Nigeria na kuwatakia uponyaji wa haraka majeruhi.

(SAUTI DUJARRIC)

‘Katibu Mkuu amesisitiza kuwa hakuna lengo la kisiasa au la kiitikadi linaloweza kuhalalisha vifo vya watu na hofu ambayo huathiri raia. Pia amesisitiza uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa serikali ya Nigeria katika mapambano dhidi ya ugaidi.’’

Msemaji huyo wa Ban amesema kuwa Katibu Mkuu amekariri kuwa makabiliano dhidi ya ugaidi lazima yazingatie haki za kimataifa za binadamu, kiutu, na sheria za wakimbizi.